MKUU WA CHUO KIKUU CHA SAUT-TABORA ANG'ARA ULAYA

Image
mkuu wa chuo kikuu cha saut-tabora(AMUCTA)
dr. Thadeus Mkamwa


MHADHIRI wa Kitanzania, Dk. Thadeus Mkamwa, amepata tuzo na kuwa miongoni mwa watafiti bora katika Bara Ulaya baada ya tasnifu yake kumuwezesha kuhitimu Shahada ya Uzamivu na kung’ara katika mashindano ya kumtafuta mtafiti bora wa mwaka 2010.

Shindano lililomuwezesha Mkamwa kupata tuzo hiyo, lilidhaminiwa na kusimamiwa na Taasisi ya Kimataifa ya Emerald, wachapishaji wa utafiti mbalimbali unaofanywa na wasomi weledi katika biashara na uchumi, sosholojia, sera na elimu kwa kushirikiana na Taasisi ya Ulaya ya Maendeleo ya Weledi wa Utawala (EFMD).

Mkamwa ambaye hivi sasa ni Mkuu wa chuo kikuu cha Archbishop Mihayo University College Tabora, tawi la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino cha Tanzania (SAUT), amekabidhiwa tuzo hiyo na mwakilishi wa Emerald katika Kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, Sibu Zondi katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Zondi Taasisi ya Emerald huandaa shindano na kutoa tuzo kila mwaka kwa kushindanisha utafiti wa wahitimu wa Shahada ya Uzamivu kutoka vyuo mbalimbali lakini mwaka 2007, 2008 na 2009 hapakuwepo mshindi yeyote kwa kuwa hapakuwepo na utafiti uliokidhi viwango kwa mujibu wa vigezo vya Taasisi ya Emerald.

“Ila mwaka huu tumempata mshindi baada ya kushindanisha tasnifu 30 zenye ubora wa kiwango cha juu katika weledi wa rasilimali watu na Dk. Mkamwa ameibuka mshindi na kupata tuzo iliyotukuka,” Zondi anasema.

Mkamwa amefanya tasnifu kuhusu Nafasi ya Mipango Kazi na Kanuni Sehemu za Kazi zinavyowezesha ufanisi wa kampuni na wafanyakazi katika kampuni kubwa katika nchi ya Ireland wakati akiwa mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika chuo kikuu cha Dublin City University ambao ulimuwezesha kuhitimu masomo yake mwaka 2009.

Akizungumzia tuzo hiyo, Mkamwa ambaye pia ni Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga, anasema amefarijika kwa kuwa kazi yake imekuwa chachu na hamasa kwa wanafunzi na watafiti wa Kitanzania wenye dhamira ya kutafuta ushindani wa kiwango cha kimataifa.

“Mara kwa mara ninapenda kuwaambia wanafunzi wangu wasome kwa bidii na kujiweka katika ushindani wa viwango vya kimataifa, tuzo hii itasaidia kueleza kwa vitendo kile ninachomaanisha,” anasema Mkamwa ambaye pia hufundisha wanafunzi wa Shahada ya Uzamili na Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino cha Tanzania (SAUT), Mwanza na Dar es Salaam.

Anasema alianza kufanya utafiti huo mwaka 2005 akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Limerick - Kemmy Business School nchini Ireland, lakini mwaka 2007 alilazimika kuhamia Chuo Kikuu cha Dublin City cha Ireland pia ili kukabiliana na changamoto alizokutana nazo wakati akiisaka shahada yake ya rasilimali watu.

“Nilihama chuo ili kuwafuata wasimamizi wa tasnifu yangu…pia nilibaini kuwa nikiwa barani Ulaya ni rahisi kupata fedha za kutosha kufanya utafiti wangu kwa kiwango cha juu,” anasema Mkamwa.

Lengo la utafiti wake ni kuangalia kama mipango kazi, kanuni na sheria sehemu za kazi zinaleta tija kwa kampuni au la.

Ili kukamilisha utafiti huo, alipeleka dodoso kwa kampuni 1,000 ambazo ziliitikia mwito wa kushiriki katika utafiti huo na alihoji mameneja, maofisa utawala na maofisa wa rasilimali watu.

Hata hivyo haikuwa rahisi kupata majibu kwa kuwa wakati mwingine alilazimika kutembelea kampuni hizo na kutoa mada na wenye kampuni walitaka kujua watafaidika vipi na utafiti huo.

Matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa mpango kazi shirikishi unasaidia wafanyakazi kujua wajibu wao na kutoa uamuzi sahihi ambao utasaidia kukuza ufanisi wa kampuni ikiwa ni pamoja na kuwapatia wafanyakazi uhuru wa kutumia vipaji vyao na kutoa mapendekezo ya kuboresha kampuni.

Pia mpango kazi shirikishi unawezesha wafanyakazi kujua malengo ya kampuni kwa siku sijazo jambo litakalowapa wafanyakazi ari ya kufanya kazi kwa bidii katika hali ya utulivu pasipo kufikiria kutafuta kazi katika kampuni nyingine.

Pia utafiti huo ulibaini kuwa kampuni zenye mpango wa kuwaendeleza wafanyakazi wake kielimu, hususani elimu ya juu zinakuwa na uhakika wa kukaa na wafanyakazi wao kwa muda mrefu zaidi kuliko kampuni zinazotoa mafunzo ya muda mfupi au zisizokuwa na programu za kusomesha wafanyakazi.

Faida nyingine ya mpango kazi shirikishi ni kutoa ajira katika mpango uliowazi na unaoeleweka kwa mujibu wa kanuni za kutoa ajira, kuzingatia haki za msingi za wafanyakazi ikiwa ni pamoja na ulinzi sehemu ya kazi, bima ya afya, mishahara mizuri na marupurupu na mrejesho wa taarifa za mipango na vikao vya kampuni.

Pia matokeo ya utafiti huo yamebainisha kuwa kushirikisha wafanyakazi katika utafiti mbalimbali unaofanywa na kampuni huwawezesha wafanyakazi kuwa na ufahamu mzuri kuhusu kampuni jambo ambalo linaongeza ari ya kufanyakazi kwa bidii.

Utafiti huo pia unawataka waajiri kutambua kuwa wafanyakazi sio chombo au nyenzo ya kuzalisha mali pekee, bali ni tunu ambayo ikitumika vyema hujenga faida mara dufu na kuiwezesha kampuni kujiimarisha hata inapotingishwa na msukosuko wa kuporomoka kwa uchumi wa dunia.

Anasema kwa kuwa kanuni za kazi ni za kimataifa, Tanzania inaweza kunufaika na utafiti wake endapo kanuni mbalimbali zitaamua kuutumia kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi wa kazi nchini.

Mkamwa anataja changamoto alizokutana nazo wakati wa kufanya utafiti huo kuwa ni pamoja na kampuni nyingi kufilisika kutokana na msukosuko wa kifedha katika soko la dunia.

“Ilikuwa vigumu kushawishi kampuni kuwa na mpango kazi shirikishi unaoongeza tija kwa kuwa kampuni nyingi zilikuwa zikikabiliwa na hali mbaya kiuchumi…hata hivyo hivi sasa wataalamu wamebaini kuwa utafiti wangu unafaa,” anasema Mkamwa.

Anaeleza changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya kampuni kufilisika na kufunga ofisi hata kabla ya kukusanya dodoso za utafiti wake, jambo ambalo lilisababisha utafiti huo kuchukua muda mrefu kuliko alivyotarajia.

“Wakati mwingine nilifika katika ofisi kuchukua majibu ya maswali niliyowaachia na kukuta ofisi imeshahama au kufungwa…sikukata tamaa, niliendelea kufuatilia katika kampuni nyingine hadi nikafikisha idadi ambayo kitaalamu inaruhusiwa ili kukamilisha utafiti,” anaeleza. Anasema njia pekee ya kukamilisha utafiti ni kusoma kwa bidii, kubadilishana mawazo na watafiti au wasomi wengine juu ya utafiti unaofanya, kuwa mvumilivu, kusikiliza na kufanyia kazi maelekezo yanayotolewa na wasimamizi, kushiriki katika makongamano ya elimu pia kuongeza bidii kila unapokutana na vikwazo. Mafanikio ya utafiti wake yanatokana na msaada na ushirikiano mzuri alioupata kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania (SAUT), Chuo Kikuu cha Limerick and Dublin City College na wasomi mbalimbali hususani wasimamizi wake.

Mkamwa anawashauri wanafunzi wanaosoma nje ya nchi kuwa wabunifu na jasiri wa kufanya uamuzi sahihi kama vile kuhamia chuo kingine ili kukamilisha malengo yao badala ya kukaa katika mazingira magumu au yenye vikwazo.

Anafafanua kuwa mwanafunzi anapotumwa kusoma nje ya nchi asiogope kuwaeleza wafadhili wake juu ya vikwazo anavyokutana navyo na kupendekeza kuhamia chuo kingine kwa lengo la kukamilisha azma ya kwenda masomoni.

Mkamwa ni mzaliwa wa Tanga katika Wilaya ya Lushoto na amepata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Gare na kujiunga na masomo ya sekondari katika Seminari ya Soni ambayo alihitimu mwaka 1987. Aliendelea kuisaka elimu kwa kujiunga St. Peter’s Junior Seminary Morogoro ambako alisoma kidato cha tano na sita na kuhitimu mwaka 1990.

Baada ya hapo, alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho iliyopo Moshi kuchukua kozi ya Philosofia. Alihitimu kozi hiyo mwaka 1992 kisha kujiunga na Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo iliyopo Kipalapala Tabora kusomea theolojia.

Masomo hayo yalienda sambamba na shahada ya theolojia inayotolewa na Chuo Kikuu cha Pontifical Urbaniana kilichopo Italia na kuhitimu mwaka 1997.

Alipata upadri mwaka 1997 na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchungaji. Mwaka 2000 alijiunga na Chuo Kikuu cha Elmira kilichopo Elmira , New York, Marekani kuchukua shahada ya sosholojia na mwaka 2004 akatunukiwa Shahada ya Uzamili katika chuo hicho hicho baada ya kuhitimu masomo ya Elimu ya Sayansi.

Mkamwa anapendelea kusoma, kufundisha, kuvua samaki, kufanya mazoezi, kusafiri, kusali, kutembelea maeneo matakatifu na kubadilishana mawazo na watu mbalimbali.

Post a Comment

ads by blogger

Follow Us

Hot in week

BLOG ZINGINE

BLOG OWNER

BLOG OWNER
MESHACK JACKSON

Side Ads

Instagram

JOIN US ON TWITTER

Text Widget

Millard Ayo – Official Website

item