HICHI NDICHO CHANZO CHA ZITTO KUUTAKA URAIS
https://menacotz.blogspot.com/2012/03/hichi-ndicho-chanzo-cha-zitto-kuutaka.html
WANAOPINGA KUONDOLEWA KWA KIKWAZO CHA UMRI WA URAIS WATOE HOJA
Sabatho Nyamsenda
Labda nitaje mapema kabisa kuwa mimi naupinga mjadala huu kwa lengo na namna unavyoendeshwa, aina ya watu wanaoushadadia, na baadhi ya hoja zinazotolewa. Lakini sipingi kuondolewa kwa vikwazo vya watu kugombea nafasi za kisiasa vikiwemo vigezo vya vyama na umri.
Mimi
si shabiki wa nadharia za kibwanyenye. Lakini wananadharia wa
kiliberali wanasema kuwa binadamu kwa asili yake amezaliwa na uhuru
kamili ambao haupaswi kuingiliwa na mtu ama taasisi yoyote. Binadamu
anapaswa kuwa mwamuzi wa maisha yake mwenyewe na kuzitumia fursa alizo
nazo pasi na kuingiliwa. Mtu anayenyimwa uhuru ama fursa, haijalishi
kama anaitumia ama la, anashurutishwa na kuonewa [‘she or he is being
coerced’]. Hivyo, yule anayemnyang’anya mtu uhuru na fursa alizonazo
anapaswa kujitetea na kuthibitisha uhalali wa kufanya hivyo.
Katika
nchi yetu, tulikuwa na kiongozi mahiri na shupavu, lakini ambaye mara
nyingi aliziminya fursa na uhuru wa watu kwa sababu mbalimbali, ikiwemo
kujenga umoja wa kitaifa na hata kujiimarishia mamlaka ya kuwa Rais
mfalme. Mtu huyo ni Mwalimu Nyerere. Na kila mara alipowanyang’anya watu
uhuru wao alijenga hoja juu ya kwa nini amefanya hivyo. Alifuta vyama
huru vya wafanyakazi, akafuta vyama vya upinzani, akafuta ushirika,
akawanyima watu fursa za kutajirika na kuwanyonya wenzao, akaminya uhuru
na fursa za kuiba fedha za umma na kula rushwa, n.k. Lakini alijenga
hoja ambazo waliozipinga waliishia tu kusema, “Ah! Hana lolote huyo,
anataka tu kujiongezea madaraka.” Na baadae alikiri kuwa baadhi ya vitu
alivyofanya vilikuwa na makosa ikiwemo kufuta ushirika.
Historia
ya dunia inatufundisha kuwa binadamu amenyimwa uhuru kwa namna
mbalimbali. Kuna wakati wanawake hawakutambulika kama binadamu. Hata
walipotambulika hawakupewa fursa za kupiga kura, achilia mbali kugombea
na kumiliki mali. Lakini baada ya ‘mapambano’ sasa dunia inakiri kuwa
wanawake ni binadamu na wanapaswa kuamua hatma zao kwa namna mbalimbali
ikiwemo kupiga kura na kugombea. Watu weusi vivyo hivyo. Lakini sasa
dunia inatambua [hata kama ni kwa unafiki] kuwa nao ni binadamu.
Masikini vivyo hivyo, lakini sasa japo wanaruhusiwa kupiga kura na
kugombea, haijalishi kama wana uwezo wa kushinda.
Hoja
niijengayo hapa ni kwamba waliowanyang’anya – na wanaotetea –
Watanzania wenye chini ya miaka 40 fursa ya kugombea urais sharti
wajenge hoja zenye mantiki na zenye kushawishi. Kwa nini ni 40 na si 39
ama 25? Ni katiba gani inayotaja umri wa kuanzia lakini haiweki kikomo?
Kuna vigezo gani vya kisayansi, kihistoria ama kimantiki vinavyoweza
kuthibitisha kuwa mtu mwenye miaka 40 atafaa zaidi kuwa Rais kuliko
mwenye 37 au 29?
Ukizipitia
kwa umakini hoja za wapingao umri kupunguzwa utagundua namna zilivyojaa
chembechembe za uhafidhina. Kwanza wapo wasemao chini ya miaka 40, mtu
anakuwa bado ni mchanga, kijana, n.k. Lakini hawatuambii kama mtu
akifikisha 40 ndio anakuwa amekua na kukomaa. Wala hawaikemei Katiba
kutoweka kikomo, kiasi kwamba hata ‘kikongwe’ mwenye miaka 120 ana haki
ya kugombea urais, lakini si ‘kichanga’ mwenye miaka 39.
Wapo
wanaotumia jina la Mwalimu kuthibitisha ‘uharamu’ wa hoja zao. Kuna mtu
alitolea mfano wa mwaka 1995, Mwalimu alipomwambia mmoja wa wagombea wa
urais kupitia CCM, kuwa, ‘Wewe bado ni mdogo. Subiri kwanza ukue’.
Lakini mtu huyo [tumwite ‘Bwana Mdogo’] alikuwa na miaka 45 wakati huo.
Mwalimu mwenyewe hakuzuiliwa kugombea urais wa TAA na baadae TANU na
kuongoza harakati za ukombozi licha ya udogo wake kiumri. Nijuavyo mimi,
sina hakika kama Mwalimu angebadili mawazo yake, iwapo angekuwa hai,
mwaka 2005 pale ‘Bwana Mdogo’ alipojitokeza tena, akiwa na uzoefu mkubwa
zaidi na umri wa miaka 55. Angalau karibu nizungumzaye nae ananiambia
udogo na uchanga wa ‘Bwana Mdogo’ huyo si wa umri, ni wa uwezo.
Lakini
Mwalimu alimshabikia mgombea fulani, ambae alikuwa ni mwanafunzi wake
na baadae kafanya nae kazi kwa ukaribu, akimpa nafasi mbalimbali ikiwemo
ile nyeti kwa wakati huo, ya uwaziri wa mambo ya nje [tumwite ‘Bwana
Msafi’]. Kuna ushahidi wa wazi kuwa kati ya watu waliomsoma na kuonekana
kumshiba Mwalimu ni huyo ‘Bwana Msafi’. Sote tumeshuhudia alikoipeleka
nchi na jinsi alivyogeuza nchi shamba la bibi: kila aliyehitaji
kujifunza kuiba kwa namna mbalimbali, ikiwemo wizi uliohalalishwa
kisheria [ubinafsishaji na uwekezaji] na ule ulioharamishwa kisheria
[EPA, Radar, Kiwira], alipata fursa katika kipindi cha ‘Bwana Msafi’. Ni
katika kipindi hicho pia tulipojifunza kuwa Ikulu ni mahali pazuri na
kuanzishia biashara, kuombea mikopo, kujiuzia bure migodi na ardhi na
kumfungulia bibie kaserikali kake ka pembeni – ‘kaenijioo’.
Lakini
‘Bwana Msafi’ na ‘Bwana Mdogo’ wote ni watu waliolelewa katika Chama,
tena angalau wakati ule ambapo Chama kiliwajali na kuwasikiliza wanyonge
wake. Wote ni watu walioingia madarakani wakiwa na zaidi ya miaka 50!
Wote ni watu waliopata fursa ya kufanya kazi, kuzungumza, kucheka, kula,
kushikana mikono na kukumbatiwa na Mwalimu; baadae wakamwona alivyougua
na kufariki, hatimaye akazikwa. Kwa maana hiyo, wanajua kabisa kuwa
Mwalimu alikuwa ni binadamu wa kawaida [aliyezaliwa, akakua, akazeeka,
akaugua, akafariki] na si malaika aliyeshushwa toka mbinguni. Hivyo,
historia inatuthibitishia kuwa hoja ya ukubwa wa umri, uzoefu na
kulelewa katika Chama haina mashiko. Na je, kuna chama gani hapa
Tanzania kiwaleacho, kwa nadharia na vitendo, watoto na vijana ili wawe
viongozi baadae? Bado tunazungumzia suala la makuzi ya kichama hata
katika zama hizi ambazo watu wanadai uhuru mpana wa kugombea urais na
ubunge bila dhamana ya vyama?
Wanaotaka
kuondolewa kwa vikwazo vya umri wanatutaka tusome historia ya Afrika,
toka DRC hata Libya: Je, Ghadafi aliingia maradakani na miaka mingapi?
Tazama jinsi alivyoibadili nchi ile akiwa kijana mdogo tu mwenye umri wa
miaka ishirini na ushee. Lakini Ji-Ghadafi zee lilikuwa tayari limeanza
kulewa madaraka na kuurejesha mfumo wa kifalme lililoupindua. Wapo
wanaotutaka kulinganisha hawa wafuatao na kusema yupi alikuwa bora
zaidi, kama tunafuatilia historia zao: Komredi Yoweri K. Museveni wa
miaka ya 70 na Mhe. Dk. Yoweri K. Museveni wa miaka ya 2000.
Lakini mjadala huu una hatari kubwa sana kama wanavyodai wanaopinga namna
hoja ya akina Zitto inavyopenyezwa. Ni mjadala unaogusa hisia na
kujaribu kuwafanya vijana wajione wao ni kundi moja, kundi
linalounganishwa na umri. Ni kipi kimfanyacho kijana mlalahoi wa
Nyamitwebili ajione kuwa yeye si sawa na walalahoi wenzake wenye umri wa
zaidi ya miaka 40, eti kisa ni wazee? Halafu ajione yuko sawa na
Januari na Zitto, eti kisa ni vijana?
Ukweli
ni kwamba vijana waliobebea hoja hii hawaishi maisha ya vijana wa
mtaani, wala hawayasikii machungu yao, zaidi tu ya kubeba hisia zao.
Kwangu mimi, sidhani kama ni sahihi kutumia kigezo cha umri kutengeneza
kundi. Kijana mwenye umri wa Zitto Kabwe au Januari Makamba ana kipi
kinachofanana nao? Januari ana chimbuko la tabaka la walala-heri. Mahali alikosomea, maisha aliyoishi na fursa alizopata zinadhihirisha wazi jinsi tabaka la walala-heri linavyoweza kujizalisha na kujiimarisha kwa namna mbalimbali. Nitaeleza.
Tuchukulie
mfano wa Zitto, ambae ana chimbuko la familia ya kilala-hoi, lakini
sasa, kwa sababu ya elimu na nafasi yake, alishaliaga tabaka hilo. Ana
utangamano upi na yule kijana waliyemaliza wote darasa la saba, ambae
sasa ni mvuvi wa kutumia mtumbwi? Je, wakikutana wana kipi
kinachofanana? Nadhani wanatofautiana kila kitu: namna na idadi ya lugha
wanazozungumza, nchi walizotembelea, aina ya vyakula walavyo, mavazi
wavaayo, nyumba waishizo, n.k. Hata ndoto waotazo na mawazo wawazayo ni
tofauti. Wakati mmoja akiwaza juu ya jinsi atakavyomalizia shahada yake
ya uzamivu huko Uropa, [...], safari yake nje ya nchi na Rais, [...];
mwingine anawaza juu ya nyavu zake zilizokamatwa na kuchomwa moto na
Magufuli (wakati huo), mtumbwi wake uliotoboka, nyumba yake ya tope na
nyasi inayokaribia kuanguka, kijishamba chake alichoporwa kupisha
mwekezaji-papa au mtoto wake aliyefukuzwa shule kwa kukosa ada ya elfu
kumi. Hawatangamani kamwe. Mmoja akiugua kichwa analazwa wodi ya ‘very
important person (V.I.P.)’ na kesho yake kupelekwa nje kwa matibabu
zaidi; mwingine huishia katika kijituo cha afya cha akina ‘poor innocent
victim (P.I.V.)’ ambacho hakina hata ‘panadol’. Hakuna utangamano.
Mmoja akijisikia kuchoka anaweza kuamua kupanda ndege kwenda Afrika
Kusini kwa mapumziko, mwingine ataishia chini ya mwembe kusinzia.
Ipo
hoja ya pili, vijana hawa wana ndoto za kuwania urais. Angalau Januari
amekwisha sema kuwa, kwanza hana ndoto hiyo, na pili, hata angekuwa
nayo, mwaka 2015 atakuwa na umri wa miaka 41. Hivyo, kama hiyo ndiyo
ingekuwa nia yake, basi asingekuwa na haja ya kuanzisha mjadala huu.
Lakini si ajabu kusikia watu wakikana ama kusema hawagombei lakini
baadae wakagombea kwa sababu wananchi au wazee ‘wamewalilia’. Zitto,
alikwishanukuliwa zamani kuwa angegombea urais ifikapo 2015. Alipoulizwa
itakuwaje, wakati utakuwa na umri ‘mdogo’ wa miaka 39 alijibu kuwa
anategemea katiba itakuwa imebadilishwa na kuondoa kikwazo hicho.
Mdogo
wake Januari aitwae Thuwain, aliwahi kuandika waraka [upo kwenye
mtandao] akiwalaani Watanzania kwa kumdharau Rais Kikwete na kumtupia
lawama kila kukicha. Alimsifu Rais kuwa ni kiongozi shupavu na amefanya
maendeleo mengi, ambayo aliyashuhudia kwa siku 90 tu alizokaa hapa
nchini kwa kipindi chote cha awamu ya kwanza ya Rais Kikwete (2005 -
2010). Na akawapa Watanzania dawa ya matatizo yao: chanzo cha matatizo
yao ni kizazi kilichozaliwa kabla ya uhuru. Hivyo, suluhisho pekee ni
kuhakikisha kuwa katika uchaguzi mkuu wa 2015, mtu yeyote aliyezaliwa
kabla ya 1961 asipate nafasi yoyote ya uongozi. Kijana aliyekaa nchini
kwa siku 90 katika kipindi cha miaka mitano, kipindi ambacho baba yake
na kaka yake walikuwa wateule wa Rais, angewezaje kuona ubovu wa utawala
uliopo, achilia mbali kufahamu machungu ya walalahoi hadi kuwapa
suluhisho?
Hoja
hii ya Thuwain ndiyo inayopenyezwa na akina Zitto na Januari katika
mjadala. Wala haikuanza leo. Januari alianza kuipenyeza hoja hiyo hata
kabla ya 2010. Zitto pia. Wanadai kuwa sasa ni wakati wa vijana. Wazee
ndiyo chanzo cha matatizo, waiachie nchi kwa vijana. Ndani ya UVCCM pia
wapo vijana, akina Salum, wamebeba bango hilo: Rais awateue wao vijana
kuwa wakuu wa wilaya na mikoa, na Chama kiwateue kuwa makatibu wa wilaya
na mikoa kwa sababu wazee wameshindwa!
Kwa
namna yoyote kinachopandikizwa hapa ni sumu ya ubaguzi – ubaguzi wa
umri. Katika mfumo wa kandamizi na wa kinyonyaji tulionao, uliowafanya
watu kupoteza matumaini, ni rahisi sana kupandikiza sumu ya aina hiyo na
ikafanya kazi. Kama
hoja ya leo ni umri, kesho itakuwa ni dini. Tuna hoja gani ya kumjibu
atakayetushawishi kuwa nchi hii imetawaliwa na wakatoliki wawili na
waislam wawili katika kipindi cha miaka 50 na hakujawahi kuwa matumaini?
Kisha akituambia kuwa chanzo cha matatizo yetu ni hizo dini mbili, na
kwamba ni wakati sasa wa kuwajaribu waprotestanti au wapagani,
tutakataa? Akija mwingine akatuambia chanzo ni makabila yaliyotawala na
kwamba sasa ni wakati wa kuwajaribu wahaya, wasukuma, wanyakyusa au
wachagga tutakataa? Na, je
atakayetuambia chanzo ni kutawaliwa na watu wasio na Phd za darasani?
Na, vipi atakayesema kuwa chanzo ni kuwa marais wote walikuwa wanaume,
na kwamba sasa ni wakati wa kumjaribu mwanamke?
Mjadala
ulioasisiwa na Zitto na Januari una lengo la kununua hisia za wanyonge
na kuwafanya wasihoji chanzo cha ufukara wao na kudadisi sababu za
utajiri wa wenzao; waendelee kutawaliwa na kunyonywa na kijitabaka
kilekile ambacho kinazidi kujizalisha; na wasiweze kujenga umoja ili
kukipindua kijitabaka hicho kinachokumbatia mfumo kandamizi wa uliberali
mambo-leo.
Kama nilivyosema, binafsi sipingi kuondolewa kwa vikwazo vya watu kugombea nafasi za kisiasa vikiwemo vigezo vya vyama na umri. Lakini si uhaini kuasisi mjadala wa aina yoyote ule kwani sasa ndio wakati wake hasa. Tunaojiita ‘watetezi’ wa maslahi ya wanyonge tunapaswa kuonyesha sura halisi za mijadala hiyo, na kuitetea au kuipinga kwa hoja!
Sabatho Nyamsenda,
Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Siasa,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
CHANZO:
Post a Comment