CHOMBEZO: GUBERI LA KIMANYEMA


MTUNZI: INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)

SIMU: 0713 59 35 46/0755 04 05 20


SEHEMU YA KWANZA


ALIPOCHEKA, alipendeza. Tabasamu lake zuri, tabasamu linaloshawishi na kusisimua, huwafanya watu hususan wanawake, wamsogelee na kumsalimia. Baadhi ya wanawake hao husisimkwa miili pindi tu waisikiapo sauti yake. Alikuwa na sauti ya kipekee, sauti iliyogusa hisia zao na kuamsha gharika la maraha kwenye michipuo ya fahamu zao.
Alikuwa ni kijana wa kiume, mwenye sura ya ucheshi na macho ya upole. Hakuwa mwoga wa kutazamana na mtu, lakini hakupenda kutazamana na mwanamume mwenzake. Kwake, macho ya mwanamume mwenzake yalikuwa na kitu asichokijua, kitu kisichopendeza.
Hali hiyo ilikuwa kwa wanaume tu, siyo kwa macho ya wanawake. Aliyapenda macho ya wanawake na ilipotokea akakutanisha macho na kiumbe yeyote wa kike, katu hakuyabandua macho yake. Ndani ya mboni za mwanamke yeyote kulikuwa na kitu fulani kisichoelezeka, lakini kilichomvutia na kumsisimua.

*****

ALIPOZALIWA wazazi wake walimpa jina la Maftah, jina ambalo baada ya miaka kadhaa lilipotea na kuzaliwa kwa jina jingine, Kiwembe, ambalo alipachikwa kutokana na yale ayapendayo na ayatendayo, yale aliyokwishayageuza sheria badala ya kawaida.
Ni katika kitongoji cha Ujiji mjini Kigoma ambako Kiwembe alizaliwa. Wazazi wake walikuwa na nyumba katika Kata ya Kasingirima, na katika ndoa yao walibahatika kupata mtoto mmoja tu, huyo Kiwembe.

Post a Comment

ads by blogger

Follow Us

Hot in week

BLOG ZINGINE

BLOG OWNER

BLOG OWNER
MESHACK JACKSON

Side Ads

Instagram

JOIN US ON TWITTER

Text Widget

Millard Ayo – Official Website

item