HATIA--- 14

HATIA--- 14

MTUNZI: George Iron.

CONT: 0655 727325


SEHEMU YA KUMI NA NNE

"Hapana sivyo!!! ila huyo John huyo John Mapulu namfahamu hana uwezo wa kuzaa iweje useme mkewe ana ujauzito?" aliuliza kwa sauti ya chini Rashid, macho yakamtoka Minja akabakia na pande la nyama mdomoni bila kutafuna, kauli ile ilikuwa imefungua akili yake kwa kiasi kikubwa.

Akatulia hivyo kwa sekunde kadhaa bila kusema lolote. Kisha akatikisa kichwa kumaanisha kuwa ametambua jambo. Akili yake ilifanya kazi harakaharaka tamaa ya pesa ya kichaga ikamwingia, ikamtuma kumchenga Rashid ili aweze kula peke yake.

"Ah!! wanawake wa mjini hao, hebu achana naye" alisema Minja. Rashid akaafiki, baada ya nusu saa wakaagana. Safari hii kila mmoja aliondoka kivyake.

ENDELEA>>>>>>



****

Matha baada ya kumhadaa Minja na kumsimamisha kazi aliamua kutokuwa mbinafsi na kumshirikisha suala hilo Michael ambaye mara nyingi alikuwa msikilizaji. Lakini katika maongezi ya siku hiyo hakuwa ameridhia maamuzi hayo yaliyotaka kufanywa na Matha, yaani kumtafutia kazi nyingine Minja ili kumuweka mbali na John.
"Na vipi siku akikutana na John, au akimpigia simu???" aliuliza Michael, Matha akakiri kuwa hali bado ni tete.
"Minja sio mropokaji ni muelewa sana" alijaribu kutetea Matha, Michael akakubali kwa shingo upande.
"Akithubutu kunichezea nitamuua!!!" alijisemea kwa sauti ya chini lakini Michael aliweza kumsikia.
"Kuliko kuua ni heri tutoroke Matha!!" alishauri Michael, Matha akamkazia macho, Michael akawahi kukwepesha macho yake. Matha akaaga na kuondoka, John na Bruno hawakuwa nyumbani.
Huo ni uoga wa kunguru!!! Akawaza Matha juu ya kauli ya Michael kuhusu kutoroka.

****

Ukaidi wa Minja mbele ya John ilikuwa dharau kubwa sana, John alijua lazima kuna kitu, hisia za kwamba Minja anaweza kuwa 'informer' na huenda ameishtukia dili yao ya kwenda kuiba Supermarket. John akawaeleza wasiwasi huo wenzake, hisia za John zikawashtua wenzake, mara moja msako Minja ukaanza. Sehemu ya kwanza kabisa ilikuwa kazini kwa Minja yaani sheli ambapo hakuwepo. Msako haukuishia hapo lilikuwa jeshi la watu wanne wenye mioyo ya kuua.
Minja alikuwa katika hatia asiyoitambua.
John alikuwa amekerwa sana na dharau aliyofanyiwa. Msako huu kwa upande wa John ulikuwa kwa faida ya Matha, alitaka kujua kuwa ni kwa jinsi gani Minja amemfahamu Matha tena kwa majina yote mawili kiufasaha.
"Au Matha ana uhusiano naye jamaa ananifanyia jeuri!!!" alihisi John, wivu ukachukua nafasi yake ukaanza kuikwaruza nafsi ya John, hasira ikajikaribisha katika kiti kilichokuwa wazi katika moyo wake.
"Nitamuua kwa mkono wangu!!!" aliapiza baada ya kumkosa pale sheli kwa mara ya tatu.
Wenzake na John walichukulia kuwa hizo ni hasira za kawaida ambazo John alikuwanazo lakini haikuwa hivyo ni wivu wa mapenzi ulikuwa unamshambulia tena shambulio la nguvu na la ghafla.
Msako ukatoka pale sheli na kuhamia nyumbani kwake, ramani ilikuwa tayari mkononi mwa kundi hili.
Wakashauriana waende usiku!!!!

*****

Kitanda kilikuwa hakilaliki, si kwa sababu ya godoro lililokuwa limechakaa sana bali kutokana na mgogoro wa nafsi, mke wa Rashid aliigundua hali hiyo kwa mumewe ambaye siku hiyo alipendezesha chumba kwa harufu ya bia tofauti na siku nyingine ambazo hunuka pombe za kienyeji.
"Baba Karim!!!....vipi mbona hulali"
"Sina tu usingizi mke wangu" alijibu kwa sauti ya kukwaruza.
Rashid alikuwa katika dimbwi kubwa la mawazo baada ya kupata taarifa kutoka kwa Minja. Umasikini ulikuwa unamtia katika fedheha kubwa, alidharauliwa na wala hakupendwa na mtu yeyote maana hakuwa na msaada wowote kwao. Wazo la utajiri kupitia kuusema ukweli unaomuhusu mke wa John lilimwingia lakini kisu kilikuwa kimeshikiliwa na Minja. Tamaa ikamwingia Rashid akatamani akishike yeye kisu hicho.
"Nitamweleza Minja na kama akikataa je?" alijiuliza.
"Akikataa nitaenda mwenyewe kwa John Mapulu" alijipatia jibu.
Mgogoro mkubwa wa nafsi ukautwaa usingizi wake, maumivu ya kichwa yakayeyusha usingizi wake. Rashid akaamua kuamka na kukaa kitandani, wakati huo mke wake alikuwa amelala tayari.
Nimeuchoka umasikini!!! alisema kwa nguvu kisha akajaribu tena kuutafuta usingizi.
Safari hii usingizi ulimchukua.
Siku iliyofuata akaamua iwe siku ya vitendo hakutaka kuchelewa zaidi. Kwa kuwa alipajua nyumbani kwa Minja aliamua kwenda usiku baada ya kuwa ametoka lindoni majira ya saa kumi na mbili jioni.
Siku nzima lindoni Rashid alikuwa anatazama vitu vya thamani huku akiamini kuwa iwapo Minja atakubaliana naye basi baada ya muda mfupi atakuwa na uwezo wa kuvinunua.
Ujio wa Minja nyumbani kwake siku moja iliyopita ulimzidishia tamaa zaidi ya kuipata pesa, miaka yake 40 aliyokuwanayo bado ilimruhusu kuwa na tamaa za kimwili, Rashid aliwatamani wanawake waliokuwa wakipishana katika maduka mbalimbali kununua vitu vya gharama.
"Nikizipata hawa watakuwa wananiheshimu na pia watakuwa wakinisalimia, hebu tazama wanavyonipita kama hawanioni vile!!!" Aliwaza Rashid, donge la hasira likamkaa kooni akajilazimisha kumeza mate lakini hayakupita. Akasonya!!
Alitamani jioni iweze kufika aijaribu bahati yake ya kupata pesa.
Jioni ilifika akaaga na kurejea nyumbani, hapo pia hakukaa sana alimuaga mkewe kuwa anatoka kisha akatoweka!! Hakusema anakwenda wapi.



*****


Chumba cha Minja kilikuwa kimya sana wakati anaingia, alijaribu kuita lakini hakupewa jibu lolote, lile giza lilimlazimu kutumia simu yake ya tochi kuweza kuona vyema ndani.
Chumba kilikuwa na harufu nzuri za manukato jambo ambalo halikuwa kawaida hata kidogo.
Jeuri ya pesa!!! aliwaza Rashid huku akichukua nafasi na kukaa.
Baada ya dakika kadhaa pakiwa na giza hivyo hivyo alisikia vishindo vya watu vikiingia ndani. Miale mikali ya tochi ilitua katika macho yake, alitumia viganja vyake kujikinga.
Maumivu makali katika paji la uso wake aliyasikilizia huku mwili wake ukiwa ardhini.
"Kwa nini leo hujaingia kazini??, kwa nini umeacha kazi tangu tufike siku zile??" Alisikia maswali yakimuelekea.
"Ni juzi tu ndio sijaenda jamani!!! sijaacha kazi, hata leo mchana nilikuwepo" alijitetea.
John alipatwa na ghadhabu akiwa nje ya chumba kile akiangalia hali ya usalama.huku akipuliza sigara yake.
"Fala huyo anawadanganya!!!" alikoroma kwa sauti ya hasira tena yenye kisilani, wivu juu ya mpenzi wake ulimtwaa kwa kiasi kikubwa. Aliamini kuwa yule ndani ya chumba kile alikuwa ni Minja.
Waliokuwa wameingia ndani waliposikia kauli inayoitwa kudanganywa moja kwa moja wakajua kuwa aliyekuwa mbele yao ni adui.
Dakika tano pekee zilitosha kumbadilisha Rashid na kuwa tayari kwa kuhamia kaburini. Ilikuwa ni kabali baabkubwa iliyomzidi nguvu mlinzi huyu ambaye hata chakula cha usiku alikuwa hajapata.
Timu nzima ya John ikajua kuwa imemuangamiza Minja.
Tamaa zikawa zimemponza Rashid, utajiri alioutaka ukawa umeingia shubiri. Mchezo asioujua mwanzo wake ukawa umetwaa uhai wake.
Rashid akatokomea na tamaa yake!!



Post a Comment

ads by blogger

Follow Us

Hot in week

BLOG ZINGINE

BLOG OWNER

BLOG OWNER
MESHACK JACKSON

Side Ads

Instagram

JOIN US ON TWITTER

Text Widget

Millard Ayo – Official Website

item