SITAISAHAU facebook
https://menacotz.blogspot.com/2012/11/sitaisahau-facebook_9.html
MTUNZI: Emmy John P.
CONTC: 0654 960040
SEHEMU YA SITA
ILIPOISHIA
Sasa na mimi nikaanza kuhaha, kana kwamba niliyoyawaza ni sahihi. Upesi nikanunua muda wa maongezi nikampigia tena rafiki yake John. Nikamsihi anieleze nini kimetokea.
Bila kusita akaanza kunieleza. Mwishowe nikapata jibu kamili. John hakuwa ameathirika na UKIMWI bali mshtuko. Joyce aliyeanguka wakati wa kuaga mwili wa marehemu viwanja vya
Raila Odinga na yeye amefariki.
Cha ajabu na kushtua hakuna ugonjwa wowote uliohusika katika kifo hicho. Nilifadhaika nikakaa chini, sikukumbuka hata kuaga tayari nilikuwa nimekata simu.
Mbona hivi vifo vinakuja mfululizo kiasi hichi?? Nilijiuliza na hakuwepo timamu yeyote wa kunijibu.
***UTATA…….Vifo hivi vinasababishwa na nini???
*** Isabella anahusika vipi??
ENDELEA...
Jesca naye kama ilivyokuwa kwa aliyetangulia aliagwa na wanafunzi uwanja uleule wa Raila Odinga. Halikuwa jambo la kushangaza bali lilimezwa na huzuni. Haikuwa mara ya kwanza vifo kutokea katika maisha ya chuo, lakini hichi kifo cha Jesca kilikuwa cha ghafla mno. Iliuma sana!!!
****
Wiki mbili zilikatika tangu Jesca aache simanzi kubwa katika chuo cha Mtakatifu Agustino. Nilikuwa karibu sana na John nikimfariji kwa kumpoteza mpenzi wake. John kwa kiasi kikubwa sana alifurahia ukaribu wangu kwake. Kiasi kikubwa upweke ukawa unatoweka.
USIKU WA MANANE
Kila kona ya jijini Mwanza ilikuwa imetulia, upepo ulikuwa unavuma kiasi cha kuyumbisha miti midogomidogo iliyoota pembezoni mwa barabara. Magari machache yalikuwa yakiipa usumbufu barabara ya lami ambayo ilikuwa katika mapumziko baada ya suluba ya mchana.
Gari dogo aina ya Corolla ilipata hitirafu ambayo ilionekana kuwasumbua vichwa abiria waliokuwa ndani yake. Kila mmoja alionekana kumsukumia mwenzake mzigo wa kutafuta suluhu ya ya gari hilo. Wale abiria watatu wote walikuwa wanafunzi wa chuo cha mtakatifu Augustino.
Baada ya muda wa kujadiliana hatimaye mwanafunzi mmoja aliyetambulika kwa jina la Joseph alivua shati lake akaweka pembeni akaingia katika ufundi. Wenzake wawili walitulia wakimtazama.
Baada ya dakika kadhaa mwanafunzi mmoja alibanwa haja ndogo. Taratibu akajivuta kichakani. Sijui kwanini aliamua kukitafuta kichaka cha mbali wakati usiku ulikuwa mnene na hapakuwa na watu wakipita hovyo. Alikifikia kichaka taratibu akaanza kuifungua zipu yake tayari kwa kukidhi haja yake ya wakati huo.
Ghafla aliiachia suruali yake na kutazama mbele katika namna ya kukodoa huku akiwa na hofu kuu. Alikuwa akitetemeka huku akifanya namna ya kushtua kama anatisha kitu kibaya kinachomkabili. Nilitamani sana kujua ni nini hicho mbele yake lakini nikaendelea kuwa mtazamaji wa filamu hiyo ya ajabu.
Kisha kama aliyesukumwa akaanguka chini. Akawa anajaribu kupambana kwa kujirusha huku na huko. Alikanyagakanyaga lakini hakufua dafu. Alirusha mikono hewani, bado alionekana kukabwa ipasavyo.
Ghafla nikajiona kuwa mtu wa ajabu sana, kwa nini nashuhudia jambo hili na sitoi msaada wowote. Nikataka kupiga kelele. Lakini koo lilikuwa limekauka.
Kwanza ni filamu!! Nilijiambia tena.
Mara yule kijana akatulia tuli. Nami hapo nikashtuka!!!!
Ndoto!! Ndoto mbaya
Post a Comment