WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, amesema matatizo yanayowakabili wananchi katika kukabiliana na ugumu wa maisha na umuhimu wa kukuza uchumi, ndiyo misingi ya vipaumbele vya bajeti ya serikali mwaka wa fedha 2011/12.
Alisema lengo ni kuwezesha shughuli za uchumi na maendeleo ya jamii kufanyika kwa wakati wote, kuimarisha miundombinu ya maji, reli, bandari na kudhibiti mfumko wa bei uliosababishwa na kuongezeka kwa bei za vyakula, mafuta, umeme na gharama za uzalishaji.
Waziri Mkulo aliyasema hayo jana katika hotuba yake kuhusu hali ya uchumi kwa mwaka 2010/11 na malengo ya uchumi kipindi cha muda wa kati, mwaka 2011/12 na 2015/16.
Alisema vipaumbele vingine katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha, ni kuongeza upatikanaji chakula kwa kuhimiza kilimo, hasa cha umwagiliaji na kuimarisha hifadhi ya chakula, ili kujikinga na tatizo la uhaba wa chakula.
Hali kadhalika, kuongeza fursa za ajira na kuwanufaisha wananchi walio wengi hasa vijana ambao ni kundi kubwa kwenye soko la ajira.
Kauli hiyo ya waziri Mkulo amekuja huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa wananchi, kuhusu hali ngumu inayowakabili wengi wao na kuitaka serikali kuhakikisha bajeti ya mwaka ujao inawaondelea hali hiyo.
Katika malalamiko yao, wananchi wamediriki kusema hali ngumu ya maisha inayowakabili, inapingana na ahadi ya serikali kwamba ingefanya jitihada kuhakikisha maisha ya Watanzania yanakuwa bora.
Katika hotuba yake, Mkullo alikiri umaskini miongoni mwa wananchi haujapungua kwa kiwango kikubwa hasa kwenye kaya zinazotegemea zaidi shughuli za kilimo.
‘’Pia, ingawa uchumi ulikuwa unaongezeka, ukuaji huo ulikuwa chini ya kiwango kinachohitajika kufikia shabaha na malengo ya dira,’’ alisema waziri Mkulo na kuongeza:
“Vyanzo vya ukuaji uchumi havikuwagusa watu wengi, hususan maskini wa vijijini maeneo ya pembezoni.’’
Alisema licha ya mambo mengine, hali hiyo imechangiwa na tatizo la kushindwa kutumia kikamilifu fursa za rasilimali nyingi za asili na jiografia ya Tanzania kupakana na bahari, katika kuinua uchumi.
‘‘Tunahitaji kuboresha miundombinu hususan ya usafirishaji, ili tuweze kutumia kikamilifu fursa ya kupakana na bahari kuweza kuwa kitovu cha biashara cha kuhudumia nchi za maziwa makuu na zisizopakana na bahari,’’ alisema.
Kuhusu deni la taifa, Mkullo alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana, lilifikia dola 11,380.2 milioni za Marekani na kwamba, liliongezeka kwa dola 654.28 milioni ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2009.
Mkullo alisema ongezeko hilo lilitokana na mikopo mipya ya ndani na nje yenye masharti nafuu kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Mkullo, malipo ya deni la taifa kipindi cha robo tatu cha mwaka kilichoishia Machi mwaka huu, yalikuwa Sh803.64 bilioni.‘’Malipo ya deni la nje kwa kipindi hicho yalikuwa Sh73.66 bilioni,’’ alisema.
Post a Comment