Wanafunzi 159 wa Shule ya Sekondari Maneromango wakimbia mitihani




  Kisarawe
WANAFUNZI 159 wa Shule ya Sekondari Maneromango wametoroka kufanya
mitihani ya majaribio ya robo muhula iliyoanza juzi katika shule hiyo.
Wanafunzi hao ambao ni vidato mbalimbali kuanzia cha kwanza hadi cha nne,
ni kati ya wanafunzi 383 wa Shule ya Sekondari Maneromango waliotakiwa
kuanzia kufanya mitihani yao Machi 27, 2012 shuleni hapo.
Akizungumza katika mahojiano na mtandao wa Thehabari.com katika shule
hiyo iliyopo Kata ya Maneromango, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani,
Mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, Jonas Buheruko alisema ofisi yake
imebaini utoro huo baada ya kukusanya taarifa kutoka vidato vyote.
Akifafanua alisema hali hiyo ya utoro na hasa wanafunzi kukimbia mitihani
hujitokeza mara kwa mara jambo ambalo limekuwa miongoni mwa vikwazo vya
shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma.
Alisema taarifa zilizokusanywa siku ya kwanza kuanza kwa mitihani hiyo,
Machi 27 mwaka huu, zimebaini kidato cha nne ndiyo wanaoongoza kwa utoro
wa mitihani kwani kati ya wanafunzi 106 waliotakiwa kuanza kufanya
mitihani hiyo ya majaribio ni 45 pekee walifanya huku 65 wakiingia
mitini.
"Taarifa zangu nilizokusanya baada ya kuanza tu kwa mitihani zinaonesha
kidato cha kwanza wametoroka wanafunzi 10 kati ya 81, kidato cha pili
wametoroka 31 kati ya 103, kidato cha tatu wametoroka 53 kati ya 93
waliotakiwa kuanza kufanya mitihani hiyo," alisema Mwalimu Buheruko.
Hata hivyo alisema kitendo cha utoro wa mithani shuleni hapo sasa
kinaendelea kuwa sugu licha ya walimu kufanya jitihada za kuwafuatilia
wanafunzi na kutoa adhabu mbalimbali kulingana na taratibu za shule.
Aidha aliongeza mwaka 2011 wanafunzi 34 wa kidato cha nne kati ya 85
walikimbia kufanya mtihani wa majaribio wa Wilaya shule hapo jambo ambalo
linawakatisha tamaa walimu katika utoaji wa elimu shuleni hapo.
"Wamekuwa wakikimbia mitihani mara nyingi...tunawapa adhabu lakini wapo
radhi kufuraia adhabu unayowapa kuliko kuja kufanya mitihani...wakati
mwingine tunapozidiwa tumekuwa tukipeleka majina ya watoro kwa Mwenyekiti
wa Kijiji na Ofisa Mtendaji wa Kata lakini bado hatujaweza kudhibiti
utoro huu," aliongeza mwalimu Buheruko.
Akizungumzia hali hiyo, Mratibu wa Elimu Kata ya Maneromango, Nicolaus
Lemma amesema wamekuwa wakiwaita mara kadhaa wazazi wa wanafunzi na
kuwashtaki pale inapobainika wanachangia utoro wa watoto wao, ila tatizo
hilo si kwa sekondari pekee bali hata shule za msingi eneo hilo.
Habari hii imeandaliwa na Thehabari.com kwa kushirikiana na Mtandao wa
Jinsia Tanzania (TGNP).

Post a Comment

ads by blogger

Follow Us

Hot in week

BLOG ZINGINE

BLOG OWNER

BLOG OWNER
MESHACK JACKSON

Side Ads

Instagram

JOIN US ON TWITTER

Text Widget

Millard Ayo – Official Website

item