HATIA---- 10

 Na GEORGE IRON

“Zawadi kwa lipi kaka nililofanya”
“Jana umetumia muda wako mwingi sana kuzungumza na Matha nimeyaona mabadiliko leo mabadiliko makubwa nilikuwa na Matha asubuhi ya leo hapa!!” John alizungumza huku tabasamu likichanua katika mdomo wake.
“Aaah!! Amakweli leo nimelala sana”
“Kwa suala hilo nahitaji kukupongeza!!!”
“Usijali wewe ni kaka yangu” Michael alisema huku hasira zikiwa zimemtawala ndani ya nafsi yake pepo wa wivu akaanza kumtafuna taratibu, akaanza kuhisi Matha ni mali yake peke yake.
“Hata kama lakini unastahili zawadi” alisisitiza John. Michael hakupinga zaidi ya kukubali kwa shingo upande hiyo zawadi.
“Matha amekuja??? Muda gani na saa ngapi ameondoka?? Au mtego huu?? Eeh!! Mungu nisaidie” baada ya muda mrefu sana kupita Michael alikumbuka kupiga dua.
Au wananichora hawa kasha wanitoe kafara! Alijiuliza.



****


Hali ya utulivu ilitawala eneo hili la Nyegezi jirani kabisa na chuo kikuu cha mtakatifu Augustino maarufu kama SAUT. Pumzi na mapigo ya moyo ya wawili hawa yalisikika, mmoja akiwa anajiamini na mwingine akiwa ametekwa na uoga. Ilikuwa saa sita na nusu usiku, sauti za ndege wasiojua ubora wa nyimbo zao zilisikika kwa mbali na mara chache kuingiliwa na sauti mbaya za popo. Maumbo yao yalikuwa yanaendana walikuwa wamesimama kama vile kuna jambo flani walikuwa wanazungumza kwa siri kutokana na ukaribu wao.
Majira ya saa saba usiku mmoja alisogea na kujificha mahali na kumwacha mwenzake akivuta sigara na kupuliza moshi hewani. Michael alikuwa ameachwa na John eneo lile, uoga ulipitiliza kipimo hadi akaizoea hali ile kwa kuamini kuwa kama John angekuwa ameamua kumuua angeweza kufanya hivyo mapema na si lazima kutumia mbinu zote hizo. Lakini licha ya kujiaminisha sana, suala la kupewa zawadi eneo kama hili halikuwa la kawaida. Zawadi yangu ni kifo!!! Alijiuliza. Alitamani kumpigia simu Matha lakini akakumbuka alikuwa amepewa onyo kali juu ya kuwasha simu.
“Shika huu waya, nitakuamuru uuvute!!!!” John alimuelekeza Michael kwa sauti ya chini. Michael akatii. John akawasha sigara na kuanza kuvuta. Mara ghafla akamuamuru Michael kuuvuta ule waya hadi kwenye ki-mti kidogo kilichokuwa jirani kabisa na njia hiyo ya uchochoroni baada ya kuufunga waya huo Michael alisikia muziki kwa mbali ukizidi kusogea karibu. Kufumba na kufumbua Michael aliuzuia mdomo wake usiweze kupiga kelele. Pikipiki ilikuwa imeachana na dereva aliyekuwa anaiongoza kama hiyo haitoshi kichwa kilikuwa kinakaribia kuachana na kiwiliwili. John alikuwa ameua kwa kumtegea waya dereva wa pikipiki.
“Panda twende…” John alimwambia Michael ambaye bado alikuwa amezubaa asijue la kufanya. Kwa sauti kali ya John akawa amerejewa na ufahamu akapanda katika pikipiki.
“Bila shaka itakufaa kwa safari za hapa na pale, kifo hiki kinanikumbusha enzi hizo naanza maisha ya ujambazi!!” John alizungumza kwa sauti ya juu ili Michael aweze kumsikia, hakuwa na wasiwasi hata kidogo. Michael hakujibu kitu.
Mnamo saa nane na nusu kila mmoja alikuwa amejichukulia nafasi katika sebule kubwa kabisa. Michael hakuwa na amani lakini John alikuwa mzoefu sana.
“Zawadi yangu!!!!!! Oooops!!! Nilikuwa nimesahau” John alikumbuka zawadi aliyoahidiwa na Matha kupitia Michael.
“Mh!! Hiyo mpaka pakuche tena” alijibu Michael.
“Hapana twende hiyo pikipiki ina mafuta ya kutosha” alitoa hoja John, Michael kwa kumuhofia John akakubali.
Mwendo wa dakika kumi tayari walikuwa Buzuluga. Kama kawaida John akamwacha Michael aende mwenyewe. Siku hii hakukaa sana alirejea na bahasha na kumpatia John kisha wakaondoka kurudi nyumbani. Ilikuwa ni nguo ya ndani ya kiume!!
Asubuhi sana aliwasili mtu asiyefahamika machoni pa Michael alikuwa maalum kwa ajili ya kubadilisha namba za pikipiki ile. Zoezi lilifanyika kwa umakini na kufikia jioni John kwa uhuru wote alitoka na pikipiki ile nje akiyapita kama hayaoni magazeti yanayozungumzia kifo cha muendesha bodaboda mitaa ya Nyegezi.
John alifika nyumbani kwa Matha majira ya saa tatu usiku baada ya mizunguko mingi ya kujaribu ubora wa pikipiki ile.
Matha alitegemea ujio huo hivyo chumba kilikuwa kinanukia sana kutokana na maandalizi ya uhakika. John alipokelewa kwa upendo wa hali ya juu sana, mabusu kadhaa ya hapa na pale yalikonga sana nyoyo zao lakini hasahasa John aliyekuwa hana la kusema mbele ya Matha.
“Nakupenda Jo!!”
“Sina la kusema nadhani unajua kuwa nakupenda”
“Asante sana” alisema Matha kinafiki, huku akijua fika ana hatia ya kumsaliti John tena kwa mtu wake wa karibu Michael. Matha alimkaribisha mezani John ili wapate kwa pamoja chakula alichokuwa amekiandaa. Walijumuika kwa pamoja na baada ya hapo wakahamishia mashambulizi kitandani. John alikuwa anampenda sana Matha!!.
Vurugu hizo zilitwaliwa na usingizi baadaye hadi John alipokuja kushtuka alfajiri. Alikuwa na miadi mida ya saa nne hivyo alivaa nguo zake bila hata kuoga kwani hapakuwa na choo wala bafu la ndani kwa ndani katika chumba cha Matha.
“Mh!! Kuoga usioge yaani na Suruali unavaa hiyo hiyo??”
“He! Sasa nitavaa ipi nyingine?? Unaota nini!!”

Post a Comment

ads by blogger

Follow Us

Hot in week

BLOG ZINGINE

BLOG OWNER

BLOG OWNER
MESHACK JACKSON

Side Ads

Instagram

JOIN US ON TWITTER

Text Widget

Millard Ayo – Official Website

item