SITAISAHAU facebook
https://menacotz.blogspot.com/2012/12/sitaisahau-facebook.html
MTUNZI: Emmy John P.
MAWASILIANO: 0654 960040
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
ILIPOISHIA
Nikataka kwenda kumuangaza nje. Lakini sikuona maana hiyo nikataka
kumuita, mdomo ukawa mzito sana. Nikageuka huku na huko. Hola!!
Nikageuka tena. Hakuna kitu.
Nikajisonya!! Kisha nikaguna mwenyewe kuwa ninamtafuta mtu gizani.
Mpuuzi kweli mimi!!! Nikasogea ukutani nikaanza kupapasa. Nikakipata kiwashio, nikabonyeza. Waaa!! Pakapendeza.
Nikageuka. Waaaa!!! Mdomo wazi, mtu anakula chakula.
Pwaaaa!! Nikaachia kikopo na glasi.
Osmani!!!
Osmani anakula chakula nilichopika mimi.
“Kaa hapo sahivi jamaa si amelala au.” Aliniambia kwa sauti isiyosikika vizuri, alikuwa na pande la nyama mdomoni.
Puuuu!! Nikaanguka. Lakini fahamu zipo pamoja nami. Namtazama Osmani. ***OSMANI ni nani katika simulizi hii ya kushangaza….simulizi iliyoanzishwa na kukutana na mwanaume facebook…kanitajirisha sasa nipo katika mabalaa.
ENDELEA.
“John!!!! John!!!” Nilianza kuita kwa sauti ya juu sana. Osman alinitazama akacheka huku akijiziba mdomo. Nikaita tena. Hakuna John aliyetokea kunisaidia.
“Amelala wewe acha kelele.” Alinionya Osman ambaye sasa alikuwa amemaliza kula na alikuwa anakunywa maji. Nikamshangaa. Alikuwa ananijibu bila wasiwasi wowote.
“Unajua nini Isabela. Tulia tuzungumze, mbona haya mambo madogo tu!!.” Aliendelea kuzungumza Osmani. Kidogo nikatulia sasa, akafanya tabasamu kisha akaendelea kuongea.
“Nimefuata kitu kimoja tu hapa!! Kimoja tu.”
“Nini?.” Niliweza kumuuliza sasa. Nikijilazimisha kuwa jasiri.
“Kitambulisho changu.” Alinieleza huku akiwa amenikazia macho. Sauti yake ilisikika vyema kabisa. Hakuwa katika kutania hata kidogo.
“Kitambulisho? Kitambulisho gani?.” Nilihoji. Bado nilikuwa chini.
“Kile nilichokupa siku ile. Pale wapi sijui. Unapajua wewe.”
“Sina kitambulisho cha mtu.” Nilijibu kwa jeuri.
Kama vile jibu lile lilikuwa sawa na kumtukana aliruka akanifikia, kiganja chake kikanyooka akanitandika kofi moja. Maumivu yakapenya hadi mahali machozi yalipojihifadhi, yakatoka kwa fujo huku kilio nacho kikisindikiza.
“Sasa nadhani unaweza kuniambia. Kitambulisho kipo wapi.”
“Nilikichoma moto.” Nilijibu huku kigugumizi kikinitawala na kilio cha kwikwi.
Yule bwana akakodoa macho baada ya kuisikia taarifa hiyo.
“Umefanyaje?” aliniuliza, sikumjibu. Nilikua natetemeka sana, nilianza kumuogopa sana Osmani, kwanza niliwaza kile kitambulisho ni cha John iweje aseme chake? na kwanini siku ile alinipa akasema nilikidondosha? Mhh!! Ushirikina!! Nilianza kuamini kwenye imani hizo ambazo nilikuwa siziamini kabisa hapo kabla
Post a Comment