JAPAN YAIPA TANZANIA BILIONI 28.2 KUBORESHA BARABARA NA KILIMO, MAKUTANO YA TAZARA KUWA NA BARABARA ZA JUU KWA JUU
https://menacotz.blogspot.com/2013/01/japan-yaipa-tanzania-bilioni-282.html
SERIKALI
ya Japan imepatia Tanzania msaada wa shilingi bilioni 28.2 kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi mitatu ya uboreshaji wa usafiri jijini Dar es
salaam na kilimo hapa nchini.
Msaada huo umesainiwa (leo)
jijini Dar es salaam na Balozi wa Japan hapa nchini Masaki Okada kwa
niaba ya Japan na Waziri wa Fedha Dkt. William Mgimwa kwa niaba ya
Serikali ya Tanzania.
Akizungumza
mara baada ya kusaini msaada huo Waziri wa Fedha Dkt . Mgimwa alisema
kuwa mradi wa kwanza utahusisha upanuzi wa barabara ya Kilwa na ile ya
Bandari ambapo jumla ya shilingi bilioni 20 zitatumika katika
kukamilisha mradi huo.
Aliongeza
kuwa mradi mwingine ni ule wa ujenzi wa barabara za juu(flyover) katika
makutano ya TAZARA ambapo jumla ya shilingi bilioni moja (1) na milioni
26 zinatarajiwa kutumika katika kukamilisha mradi huo.
Dkt.
Mgimwa aliongeza kuwa eneo lingine ambalo litanufaika na msaada kutoka
Japan ni kuunga mkono sera ya Kilimo kwanza ambapo Tanzania imepata
shilingi bilioni sita(6) na milioni 92 kwa ajili ya kuhakikisha
kunakuwepo kwa usalama wa chakula cha kutosha katika maeneo mbalimbali
hapa nchini.
Alisema
kuwa upande wa eneo hilo lengo ni kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wa
kipato cha chini wanaboresha kilimo ambacho kitawahakikisha uhakika wa
chakula wakati wote na hivyo kuondokana na umaskini.
Kwa
upande wa Balozi wa Japan hapa nchini Masaki Okada alisema kuwa
wananchi wengi wa Tanzania hasa wakazi wa Jiji la Dar es salaam wamekuwa
wakisubiri kwa hamu barabara za juu ili kusaidia kupunguza msongamano
wakati wa kuja na kutoka katikati ya jiji la Dar es salaam.
Alisema
kuwa utakapo kamilika mradi huo utasaidia kupunguza tatizo la
msongamano na hivyo kupunguza saa za mwananchi kusafiri kuja na kutoka
katikati ya jiji la Dar es salaam.
Balozi
Okada alisema kuwa hatua hii itakuwa muhimu katika kukuza uchumi kwani
wananchi watakuwa na muda wa kutosha kuzalisha mali kutoka na
miundombinu kuruhusu magari kwenda kasi pasipo kikwazo.
Post a Comment