UFAFANUZI WA WAZIRI KUHUSU GESI YA MTWARA!!
https://menacotz.blogspot.com/2013/01/ufafanuzi-wa-waziri-kuhusu-gesi-ya.html
Kutoka Wizara ya Nishati na Madini:Ufafanuzi wa Kina Kutoka Kwa Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo Kuhusu Miradi ya Utafutaji na Uvunaji wa Gesi Asilia Nchini na manufaa makubwa yatakayopatikana kwa wananchi wote wa Tanzania wakiwemo wale wa Mikoa ya Mtwara na Lindi.
Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo (Mb)
--
1.0 UTANGULIZI
Wizara ya
Nishati na Madini inapenda kutoa ufafanuzi wa miradi ya Gesi Asilia
ambayo itatekelezwa kwa kushirikiana na wawekezaji katika Sekta ndogo ya
Gesi Asilia na kueleza manufaa makubwa yatakayopatikana kwa wananchi
wote wa Tanzania wakiwemo wale wa Mikoa ya Mtwara na Lindi.
Siku ya
Alhamisi, tarehe 27 Disemba 2012, baadhi ya Vyama vya Siasa vya Upinzani
viliratibu na kuhamasisha baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara, wengi wao
wakitokea Mtwara Mjini kufanya maandamano ya kudai raslimali ya Gesi
Asilia iwanufaishe wakazi wa Mtwara na kupinga mradi mkubwa wa ujenzi wa
Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Wizara ya
Nishati na Madini inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa Wa-Tanzania wote
kwa kupitia vyombo vya habari.
Tokea Uhuru,
uchumi wa Tanzania umetegemea kilimo cha mazao ya biashara kama vile
katani (Tanga na Morogoro), pamba (Mwanza, Mara na Shinyanga), kahawa
(Kilimanjaro, Kagera, Ruvuma na Mara), chai (Iringa) na tumbaku
(Tabora). Fedha za mazao haya zimewanufaisha wakazi wa mikoa yote ya
nchi yetu bila ubaguzi wo wote wala wakulima wa kutoka mikoa hiyo
hawajawahi kufanya maandamano wakidai upendeleo (dhidi ya Wa-Tanzania
wengine) wa aina yo yote ile.
1 Mapato
yatokanayo na uchimbaji wa dhahabu (Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga na
Tabora), almasi (Shinyanga) na tanzanite (Manyara) yamewanufaisha
Wa-Tanzania wote bila ubaguzi wo wote ule! Minofu ya samaki wa Ziwa
Victoria (Mara, Mwanza na Kagera) imeliingizia Taifa letu fedha nyingi
ambazo zimetumiwa na wakazi wa nchi nzima bila ubaguzi wowote.
Aidha kuna
mikoa ambayo inazalisha mazao ya chakula kwa wingi kwa manufaa ya
Wa-Tanzania wote.Mahindi kutoka Rukwa,Mbeya, Ruvuma na Iringa
yanasafirishwa kwenda mikoa yote ya nchi yetu bila kujali
eneo yanakolimwa na wakazi wa mikoa hiyo hawajawahi kudai mahindi hayo ni
kwa ajili ya watu wa mikoa hiyo pekee. Sukari ya Kilombero, Mtibwa na
Kagera inatumiwa na wakazi wa mikoa yetu yote bila ya kuwepo madai ya
mikoa inayozalisha sukari hii kupewa upendeleo wa aina yo yote ile. Maji
ya Mto Ruvu yanatumiwa na wakazi wa Dar Es Salaam bila manung’uniko yo yote kutoka kwa wakazi wa eneo la chanzo cha Mto Ruvu.
Umeme wa kutoka
Mtera, Kidatu na Kihansi (Dodoma na Morogoro), Hale (Tanga), na Nyumba
ya Mungu (Kilimanjaro) unatumiwa na wakazi wote wa Tanzania bila ubaguzi
au malalamiko ya wenyeji wa sehemu ambazo umeme huo unafuliwa na
kusafirishwa kwenye Gridi ya Taifa.
Kwa hiyo,
kutokana na mifano hii michache, ni wajibu wa wazalendo na wapenda
maendeleo wa kweli na hasa Wa-Tanzania wanaopinga ubaguzi wa aina yo
yote ile kujiuliza kwa kina sababu zilizopelekea Vyama Siasa vya
Upinzani kupanga, kuhamasisha, kushabikia na kuongoza maandamano ya tarehe 27 Disemba 2012 pale Mtwara Mjini.
2.0 RASLIMALI YA GESI ASILIA TANZANIA
Gesi Asilia
ilianza kugundulika hapa nchini tangu mwaka 1974 kwenye Kisiwa cha Songo
Songo, Mkoani Lindi. Baada ya hapo Gesi Asilia imegundulika maeneo ya
Mtwara Vijijini, yaani Mnazi Bay (1982) na Ntorya (2012), Mkuranga
(Pwani, 2007), Kiliwani (Lindi, 2008). Kiasi cha Gesi Asilia iliyogunduliwa katika maeneo haya inakadiriwa kuwa Futi za
2 Ujazo Trilioni 4.5 – 8. Katika kipindi
cha miaka mitatu iliyopita, kumekuwa na kasi kubwa ya utafutaji Mafuta
na Gesi Asilia uliojikita zaidi kwenye maji ya kina kirefu cha bahari.
Kiasi cha Gesi Asilia iliyogundulika katika kina kirefu cha maji
inafikia takribani Futi za Ujazo Trilioni 27. Kiasi cha wingi wa Gesi
Asilia yote iliyogunduliwa nchi kavu na baharini inafikia takribani Futi
za Ujazo Trilioni 35.
Kufuatana na
Sheria za nchi yetu zinazotumiwa kugawa mipaka ya mikoa iliyopo kando
kando mwa bahari (isivuke 12 nautical miles au 22.22 km kuingia
baharini), Gesi Asilia iliyogunduliwa hadi sasa katika Mkoa wa Mtwara
pekee ni asilimia 14 tu ya gesi yote iliyogundulika nchini.
Kwa kutumia kigezo hicho cha Sheria za mipaka ya ki-utawala ya mikoa
yetu, Lindi inayo 7% ya gesi yote, Pwani 1% na huku Kina Kirefu cha
Bahari (Deep Sea) ndicho chenye gesi nyingi (78%) kuliko mikoa yote
ikiwekwa pamoja! Kwa hiyo, hakukuwa na haja ya kufanya maandamano
kwa sababu Gesi Asilia nyingi inapatikana kwenye bahari ya kina kirefu
ambayo iko ndani ya mipaka ya nchi yetu bila kujali mipaka ya mikoa
yetu. Isitoshe Gesi Asilia imegundiliwa kwenye miamba tabaka
(sedimentary rocks) yenye umri wa Miaka kati ya Milioni 199.6 hadi
23.03. Mipaka ya Bara la Afrika, ya nchi yetu na ile ya mikoa
yetu haikuwepo wakati huo!
Utafutaji wa
Mafuta na Gesi Asilia pia unaendelea tukiwa wa mategemeo makubwa ya
upatikanaji wa raslimali hizi katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro,
Tanga, Manyara, Kigoma, Mbeya, Njombe, Rukwa, Katavi, Morogoro na Tabora
pamoja na kwenye kina kirefu cha maji baharini kuanzia mpaka wetu na
Msumbiji hadi mpaka wetu na Kenya. Hatutarajii mikoa hii nayo ifanye
maandamano ya kutaka kuhodhi raslimali za Gesi Asilia na Mafuta
zitakapogunduliwa mikoani mwao.
3.0 MATUMIZI YA GESI ASILIA YA MNAZI BAY (MTWARA) NA SONGO SONGO (LINDI)
Mpaka hivi sasa
Gesi Asilia inayozalishwa na kutumika nchini ni kutoka Mnazi Bay
(Mtwara Vijijini) na Songo Songo (Kilwa, Lindi). Gesi ya Mnazi Bay kwa
sasa huzalisha umeme kwa ajili ya Mikoa ya Mtwara na Lindi tu. Mitambo
ya kufua umeme kutokana na Gesi Asilia iliyopo Mtwara Mjini inao uwezo
wa kuzalisha MW 18 lakini matumizi ya umeme ya Mikoa ya Mtwara na Lindi
haijavuka MW 12. Umeme huo wa Mtwara unafuliwa na TANESCO huku Kampuni
za Wentworth na Maurel & Prom zikizalisha Gesi Asilia (inayotumiwa
na TANESCO) kiasi cha Futi za Ujazo Milioni 2 kwa siku. Ikumbukwe kwamba
ufuaji wa umeme wa hapo Mtwara Mjini ulikuwa mikononi mwa Kampuni ya
Artumas iliyofilisika.
Tangu Desemba 2006 hadi leo hii kiasi
cha
gesi kilichotumika kufua umeme kwa ajili ya mikoa hiyo miwili ni chini
ya asilimia 1 ya gesi yote iliyogundulika Mnazi Bay (Mtwara
Vijijini). Vilevile ikumbukwe kwamba kuna visima vinne vya Gesi Asilia
pale Mnazi Bay (Mtwara Vijijini) na kinachotumika kwa sasa na tena
kwa kiwango cha chini kabisa ni kimoja tu!
Aidha ni vizuri
ndugu zangu Wa-Tanzania wakaelewa kuwa Gesi Asilia hii inatafutwa na
kuchimbwa na wawekezaji wenye mitaji mikubwa, wataalamu na teknolojia ya
utafutaji na uchimbaji wa Gesi Asilia ambao wanapaswa kurejesha mitaji
yao. Uchorangaji wa kisima kimoja cha utafutaji wa Gesi Asilia nchi kavu
unahitaji Dola za Marekani Milioni 40, na kwenye kina kirefu cha maji
baharini zinahitajika zaidi ya Dola za Marekani Milioni 100. Ikumbukwe
kwamba, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Mafuta la Tanzania
(TPDC), inatumia fedha za walipa kodi wa nchi nzima kwa shughuli za
kuvutia, kuratibu na kusimamia utafutaji na uendelezaji wa Gesi Asilia
nchini kote ikiwemo Mikoa ya Mtwara na Lindi. Walipa kodi Wa-Tanzania
bado hawajalalamika wala hawajafanya maandamano ya kudai fedha zao
za kodi zisitumike huko Mtwara!
Ni muhimu pia
tukaelewa kwamba Gesi Asilia iliyopo Mnazi Bay (Mtwara Vijijini)
inazalisha umeme peke yake kwa ajili ya Mikoa ya Mtwara na Lindi. Gesi
Asilia ya Songo Songo (Kilwa, Lindi) ndiyo inayotumika kuzalisha umeme
kwa ajili ya Gridi ya Taifa, na pia kwa ajili ya wananchi wa Kisiwa cha Songo Songo (Lindi), maeneo ya Somanga
4 Fungu (Lindi)
na viwandani (Dar Es Salaam). Tangu Oktoba 2004 ambapo mitambo ya kufua
umeme ilipoanza kazi hadi leo hii, kiasi cha Gesi Asilia ya Songo Songo
kilichotumika ni asilimia 7 tu ya Gesi Asilia yote iliyogunduliwa huko.
Kwa hiyo, takwimu zinaonyesha kwamba hata uchumi wa Jiji la Dar Es
Salaam unatumia kiasi kidogo sana cha Gesi Asilia (7%) iliyopo Songo
Songo (Kilwa, Lindi). Ikumbukwe kwamba waajiriwa kwenye viwanda vya Dar
Es Salaam wamo wanyeji wa kutoka Mtwara Mjini ambako maandamano
yalifanyika na vilevile wamo wafanyakazi ambao ni wanachama wa Vyama vya
Siasa vya Upinzani vilivyopanga, ratibu na kushabikia maandamano ya
Mtwara Mjini ya tarehe 27 Disemba 2012.
4.0 MIPANGO YA MATUMIZI YA GESI ASILIA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA 5 HADI 10
(a) Ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia hadi Dar Es Salaam:
Kuuza Gesi
Asilia Jijini Dar es Salaam, kitovu cha uchumi wa Tanzania (80% ya
mapato ya nchi yetu yanazalishwa Dar Es Salaam) ni uamuzi mzuri wa
ki-uchumi. Tayari kuna viwanda 34
vinatumia Gesi Asilia ambavyo vinahitaji kupanua shughuli zao endapo
gesi zaidi itapatikana. Soko kubwa la Gesi Asilia lipo tayari Dar es
Salaam (na siyo Mtwara), ambapo ipo mitambo ya kufua umeme kwa kutumia
mafuta. Serikali inatumia fedha nyingi za kigeni kununulia mafuta ya
kufua umeme tunaoutumia kila siku.
Takribani Dola za Marekani Bilioni Moja
(sawa na Shilingi Trilioni 1.6) kwa mwaka zitaokolewa kutokana na
mitambo iliyopo nchini ikifua umeme kwa
kutumia Gesi Asilia na kuachana na mafuta ambayo ni ya bei kubwa sana.
Bei ya umeme kwa uniti moja (KWh) ya umeme unaofuliwa kutumia dizeli na
mafuta ya aina nyingine ni kati ya Senti za Marekani 30 hadi 45 na huku
bei ya uniti moja hiyo hiyo ni Senti za Marekani 6-8 kwa umeme
utokanao na Gesi Asilia na zinapungua na wakati wa matumizi. Vilevile,
takribani Dola za Marekani millioni 202 kwa mwaka zitaokolewa iwapo Jiji
la Dar Es Salaam litatumia Gesi Asiliabadala ya mafuta katika magari,
taasisi na majumbani.
5.Fedha hizi
zikiokolewa zitatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa letu kwa
manufaa ya Wa-Tanzania wote wakiwemo wale waliondamana na wale
walioratibu maandamo ya Mtwara Mjini ya tarehe 27 Disemba 2012.
(b) Umeme mwingi zaidi kutokana na Gesi Asilia:
Bomba la Gesi
Asilia linalojengwa litasafirisha gesi nyingi zaidi ambayo itawezesha
mitambo mipya itakayojengwa Kinyerezi (Dar Es Salaam) kufua umeme wa
zaidi ya MW 990. Umeme mwingine utafulia Somanga Fungu (Lindi) wa kiasi kisichopungua MW520.
(c) Usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini mwetu:
Dar es Salaam
ndiko kuna miundombinu mikubwa ya usafirishaji na usambazaji wa umeme
kuliko mikoa mingine yote, hivyo ni uamuzi wa ki-uchumi unaotulazimisha
kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara na kuipeleka
Dar Es Salaam ambako itatumika kufua umeme, na kutumika moja kwa moja
viwandani, majumbani na kwenye magari.
(d) Kwa kuzingatia mahitaji ya Gesi Asilia yatakayojitokeza:
Bomba la
kusafirisha gesi litawekewa matoleo ya kuchukulia gesi (tie-off) katika
maeneo ya Mtwara, Lindi, Kilwa na Mkuranga ili kuhakikisha kuwa miji hii
inakuwa na Gesi Asilia ya uhakika wakati wowote itakapohitajika. Kwa
hiyo kuweka mitandao ya usambazaji wa gesi kutoka kwenye Bomba la Gesi
Asilia linalojengwa kutarahisisha matumizi ya Gesi Asilia viwandani
na majumbani katika Mikoa ya Mtwara na Lindi, na kwenye mikoa mingine
kwa siku za baadae.
(e) Serikali
imetenga maeneo katika pwani ya Mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) kwa
ajili ya uanzishwaji wa maeneo ya viwanda (Industrial Parks/Estates)
vikiwemo viwanda vya
mbolea, Liquefied Natural Gas (LNG) na Petrochemicals. Ujenzi wa kiwanja cha sementi uko katika hatua za mwisho za maandalizi.
(f) Ili
kutengeneza mazingira mazuri ya biashara ya Gesi Asilia na Mafuta kwa
kampuni za huduma, malighafi na vitendea kazi, Serikali imetenga eneo
maalumu Mtwara, ambalo litawekewa miundombinu ya msingi ili kutoa
vivutio mbalimbali kwa makampuni hayo. Eneo hilo litapewa hadhi ya
Ukanda Huru wa Bandari (Freeport Zone).
Ni lazima
shughuli za kusafisha na kusafirisha Gesi Asilia zitatoa ajira katika
maeneo husika. Kwa mfano kwa mitambo ya kusafishia gesi inayojengwa
Madimba (Mtwara Vijijini) na SongoSongo (Kilwa, Lindi), kila mtambo
utahitaji wafanyakazi na wengine watatoka Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Watanzania
wanakumbushwa kuwa raslimali zilizopo nchini ikiwemo gesi asilia,
madini, makaa ya mawe, wanyama pori, misitu, milima ya utalii, mito,
maziwa, bahari n.k ni za Wa-Tanzania wote kwa mujibu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Raslimali hizi zinapatikana, zinatunzwa
na kuzalishwa maeneo mbalimbali nchini mwetu na mapato yake yanatumika
kwa maendeleo ya Wa-Tanzania wote bila kujali maeneo raslimali hizo
zilipo.
Tusikubali kuvunja nchi yetu vipande
vipade kwa kisingizio cha raslimali zilizopo mikoani mwetu. Tusikubali
kuvunjavunja mikoa yetu kwa kisingizio cha raslimali zilipo kwenye
wilaya zetu.Tusikubali kuvunjavunja wilaya zetu kwa kisingizio cha
raslimali zilizopo kwenye tarafa zetu. Tusikubali kuvunjavunja tarafa
zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye kata zetu.
Tusikubali kuvunjavunja kata zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo
kwenye vijiji vyetu na mitaa yetu.
MUNGU IBARIKI TANZANIA, DUMISHA UHURU NA UMOJA WETU
Prof Dr Sospeter Muhongo (Mb)
WAZIRI YA NISHATI NA MADINI
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Post a Comment