Zitto chupuchupu kutimuliwa CHADEMA! *Hoja ya kumng’oa yajadiliwa Baraza Kuu CHADEMA >> MMOJA APINGA KWENYE JAMII FORUM
https://menacotz.blogspot.com/2013/01/zitto-chupuchupu-kutimuliwa-chadema.html
KWA mara ya pili mfululizo, katika kipindi kisichozidi miezi sita, jitihada za siri za kujaribu kumng’oa kutoka ndani ya CHADEMA, Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe zimegonga mwamba.
Tukio la kukwama kwa mkakati huo lilitokea ndani ya kikao cha Baraza Kuu la Chadema kilichoketi juzi katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kwamba, hoja ya kutaka Zitto na Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda Magalle wavuliwe uanachama wa Chadema ililetwa na uongozi wa Baraza la Vijana la Taifa la chama hicho (BAVICHA).
Wajumbe watatu tofauti wa kikao hicho, waliozungumza na Mtanzania Jumatano walisema hoja hiyo ambayo haikuwa miongoni mwa ajenda za kikao hicho, iliibuliwa wakati wa kujadili mengineyo.
Kwa mujibu wa Bavicha, Zitto na Shibuda walishitumiwa kwa madai ya kuhatarisha uhai wa chama hicho kutokana na kile kilichodaiwa kuwa na mienendo ya kugawa viongozi na kutoa matamshi yanayohatarisha uhai wake.
Kosa jingine alilotuhumiwa nalo Zitto pamoja na Shibuda ambaye hata hivyo hakuwemo kwenye kikao hicho ni tuhuma kwamba anatumiwa na mahasimu wa chama hicho wenye lengo la kukidhoofisha kisiasa.
Wapasha habari wetu walieleza kuwa hatua ya Mbowe kuruhusu hoja hiyo kuibuka ilisababisha Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe aliyekuwa akiongoza kikao hicho alazimike kuzima kuendelea kwake baada ya mkutano kukumbwa na tafrani.
Tafrani hiyo ilisababishwa na kuibuka kwa mgawanyiko mkubwa wa kimakundi, moja likiunga mkono msimamo wa Bavicha huku jingine likiwatetea Zitto na Shibuda.
Hata hivyo, mpira ulionekana kumgusa zaidi Zitto ambaye alikuwa miongoni mwa wajumbe waliokuwamo ndani ya chuma cha mkutano wakati hoja hiyo ilipoibuliwa.
Taarifa zimeeleza kuwa, wajumbe tisa walichangia mjadala huo huku watatu kati ya hao, wakimtuhumu Zitto kwa kulifadhili genge la vijana wakorofi ndani ya Bavicha ambalo baadhi ya wafuasi wake walitimuliwa katika chama hicho hivi karibuni.
Habari zaidi zinaeleza kwamba, wajumbe wawili walipinga hoja ya kutaka Zitto afukuzwe na badala yake wakakieleza kikao hicho kwamba, shutuma zilizokuwa zikielekezwa kwake hazikuwa za kweli.
Wajumbe hao walieleza mshangao wao wa kuendelea kusakamwa kwa Zitto ambaye ni kiongozi wa juu wa chama hicho wakati kukiwa na kundi la vijana ambao wako katika rekodi za kupata kumtukana wakiachwa wakiendelea kuwa wanachama.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mjumbe kutoka Longido ambaye alionekana kutofurahishwa na mwenendo huo wa mambo, alikieleza kikao hicho kuwa, CCM kimepandikiza ugomvi ndani ya chama hicho ili Zitto aonekane mbaya.
Aliwataka wajumbe wenzake kuwa makini na njama hizo za CCM ambazo alidai iwapo zingechukuliwa juu juu zingeweza kusababisha mpasuko mkubwa wa kisiasa ndani ya Chadema.
Hata hivyo, baada ya hali hiyo kutokea, Mwenyekiti wa kikao hicho, Mbowe, ambaye alikuwa akishinikizwa na wajumbe atoe nafasi kwa Zitto kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwake, alikataa kufanya hivyo.
Hatua hiyo ya Mbowe ilipingwa na baadhi ya wajumbe waliosikika wakiguna na mmoja wao akasikika akisema kwamba, pengine viongozi wa juu wa chama hicho walikuwa sehemu ya mkakati wa kumng’oa Zitto.
Zitto mwenyewe alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alijibu kwa kifupi, “I have no comment” akimaanisha kwamba hakuwa na cha kusema kabla ya kukata simu.
Kama ilivyokuwa kwa Zitto, ndivyo ilivyokuwa pia kwa Mkurugenzi wa Habari wa chama hicho, John Mnyika ambaye hata baada ya kupigiwa simu kwa zaidi ya mara moja, hakuwa tayari kueleza lolote.
“Pengine katika hayo uliyouliza, miye binafsi sina majibu nashauri ungewasiliana na huyo aliyekupatia taarifa hizo kwa ajili ya kukupa maelezo sahihi,” alieleza Mnyika.
Kwa muda sasa kumekuwepo na taarifa za kuwapo kwa mikakati ya chini chini inayoratibiwa na wanasiasa walio ndani ya Chadema ya kutaka Zitto avuliwe uanachama au anyang’anywe nyadhfa zake zote ndani ya chama kwa kile kinachodaiwa kuwa amekuwa akitofautiana kimsimamo na baadhi ya viongozi wake wakuu.
Makada wa Chadema ambao wamekuwa wakihusishwa kushiriki mpango huo ni pamoja na wabunge wa chama hicho na maofisa wa makao makuu ambao hivi karibuni waliripotiwa kuanza kufuatalia kile walichoeleza kuwa ni mali za Zitto kwa lengo la kuzitangaza.
CHANZO : MTANZANIA JUMATANO
MPINGA HOJA ASEMA>>>>>>>.
THE GUY LOOKED AS COOL AS A LION IN A ZOO THROUGHOUT THE MEETING....
IN FACT HE SAT ON THE HIGH TABLE ITSELF! HOW DO YOU CHASE SOMEBODY FROM THE HIGHTABLE BEATS ME.....
THERE WERE NO SIGNS OF YOUR ALLEGATIONS...I WAS THERE MR INFORMER!
IN FACT HE SAT ON THE HIGH TABLE ITSELF! HOW DO YOU CHASE SOMEBODY FROM THE HIGHTABLE BEATS ME.....
THERE WERE NO SIGNS OF YOUR ALLEGATIONS...I WAS THERE MR INFORMER!
Post a Comment