HIVI NDIVYO MAN UNITED ILIVYOTILEWA NA REAL MADRID KWENYE UEFA


Siamini....! Luis Nani wa Man U akisikitika kwa kushika kichwa baada ya kutolewa na refa kwa kadi nyekundu ya utata kufuatia kumpiga teke kwa bahati mbaya beki Arvalo Arbeloa wa Real Madrid (kushoto).   
Pole dogo... hata mimi nimeona kuwa refa kakuonea!  Kocha Jose Mourinho wa Real Madrid akimfariji Mreno mwenzake Luis Nani baada ya winga huyo kutolewa nje kwa kadi nyekundu ya utata.
Washkaji Man U mnisamehe...! Cristiano Ronaldo wa Real Madrid akionekana kusikitika badala ya kushangilia baada ya kufunga goli la pili lililoipa ushindi Real Madrid dhidi ya klabu yake ya zamani ya Man U.  
MANCHESTER, England
KOCHA wa Real Madrid, Jose Mourinho amedai kwamba "timu bora zaidi imefungwa" baada ya wachezaji 10 wa Manchester United kufungwa nyumbani mabao 2-1 kutoka kwa Real Madrid kwenye Uwanja wa Old Trafford na hivyo kung'olewa katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa kipigo cha jumla cha mabao 3-2.

Man U walipata goli la utangulizi katika dakika ya 48 ya mechi hiyo ya hatua ya16-bora baada ya beki Sergio Ramos kujifunga lakini kibao kikawageukia baada ya Luis Nani kutolewa kwa kadi nyekundu ya utata kwa kosa la kumpiga teke mbavuni beki Arvalo Arbeloa wa Real Madrid katika dakika ya 58.

Hata hivyo, marejeo ya picha za video yalionyesha wazi kuwa Nani hakukusudia kufanya kosa hilo kwani alikuwa akiwania mpira na hivyo hakumuona Arbeloa aliyekuwa nyuma yake.

Baada ya Man U kubaki 10, Mourinho akamtoa Arbeloa na kumuingiza Luka Modric ambaye alitumia dakika saba tu uwanjani kuisawazishia Real Madrid kwa shuti kali la nje kidogo ya 18 katika dakika ya 66 kabla Cristiano Ronaldo hajafunga la ushindi katika dakika ya 69 baada ya kuunganisha wavuni krosi safi kutoka kwa Gonzalo Higuain.

"Sizungumzii kuhusu uamuzi wa refa kwa sababu sina uhakika kuhusiana na hilo. Tukiachana na refa, ukweli ni kwamba timu bora ndiyo iliyofungwa. Hatukucheza vizuri. Hatukustahili kushinda lakini soka ndivyo ilivyo", José Mourinho alisema wakati akihojiwa kwa kifupi na kituo cha televisheni cha 'ITV1'.

"Wakati tukiwa na wachezaji 11 v 11, nilikuwa na wasiwasi kuwa tunaweza tusishinde. Sijafurahi kwa sababu tulicheza vizuri sana dhidi ya Barcelona. Leo (jana usiku) nilitarajia makubwa zaidi. Nilisubiri kuona tukicheza kwa namna tofauti", kocha huyo wa Real Madrid alikiambia kituo kingine cha televisheni cha 'Sky Sports'.

"Mtazamo wangu ni kwamba Manchester United walikuwa wakicheza vizuri sana, walijilinda vyema na kuwa ngangari zaidi," Mourinho aliiambia 'BBC'.

"Najua Manchester United ni timu kubwa, siyo tu kimwili bali kiakili. Najua wana kocha anayeweza kuwahamasisha, lakini nilikuwa nikisubiri kuona tukicheza kwa namna tofauti."

Katika mechi nyingine ya mtoano Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya jana, Borussia Dortmund walifuzu kwa hatua ya robo fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2 dhidi ya Shaktar Donetsk ya Ukraine kufuatia ushindi mnono walioupata wa mabao 3-0 katika mechi yao ya marudiano mjini Dortmund. Katika mechi yao ya kwanza nchini Ukraine, timu hizo zilitoka sare ya 2-2.

CRISTIANO RONALDO ASIKITIKA
Ronaldo alifurahia timu yake ya Real Madrid kufuzu kwa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya lakini kamwe hakuacha kuonyesha heshima kwa klabu ya zamani iliyomkuza na kumpa nafasi ya kufikia alipo sasa.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno, alikiri kwamba ingawa amefurahia kufuzu kwao kwa kuing'oa Manchester United, amejikuta akiwa katika "wakati mgumu" pia kwa kuisikitikia timu yake ya zamani.

Ronaldo ndiye aliyefunga goli la ushindi la Real baada ya Man U kubaki 10 uwanjani kufuatia kutolewa nje kwa kadi nyekundu ya utata kwa winga mwenzake wa kimataifa wa Ureno, Nani.

"Nilifanya kazi yangu, ya kuisaidia Real Madrid kushinda, na nimefurahi sana kwa hilo... lakini nilijisikia vibaya pia. Ni hali ya kutaka kufanya kitu fulani lakini unashindwa kukifanya," Ronaldo aliiambia TVE.

"Nilicheza nikiwa Manchester United kwa miaka mingi, na kama kuna siku nitacheza dhidi ya Real Madrid itakuwa hivi pia. Kupokewa vizuri ni jambo maalum kwangu, kurudi nyumbani, kuonana na marafiki. Ndani ya moyo wangu nimefurahi lakini pia nina huzuni dhidi ya Man Utd.

Kama ilivyokuwa baada ya kufunga goli la kuisawazishia Real Madrid katika mechi yao ya kwanza iliyomalizika kwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, Ronaldo hakushangilia goli la pili lililowapa ushindi wa 2-1 jana kwa sababu ya kuiheshimu klabu yake ya zamani.

"Sikushangilia kwa sababu ya kuwaheshimu walewote walionipokea vizuri hapa (Old Trafford), lakini kitu nilichokitaka sana ni kushinda na kuendelea na ndoto ya Real Madrid ya kutwaa taji la 10 la Klabu Bingwa Ulaya," alisema Ronaldo. 

Related

UEFA 3599672210878833991

Post a Comment

ads by blogger

Follow Us

Hot in week

BLOG ZINGINE

BLOG OWNER

BLOG OWNER
MESHACK JACKSON

Side Ads

Instagram

JOIN US ON TWITTER

Text Widget

Millard Ayo – Official Website

item