ZITO AMSIFIA KIKWETE
MBUNGE wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe
(Chadema), amesema Rais
Jakaya Kikwete ni mtu wa
ajabu na kueleza kuwa kama
si uvumilivu wake nchi
ingekuwa katika machafuko
makubwa.
Zitto ametoa kauli hiyo juzi,
wakati akizungumza katika
Kipindi cha Makutano
kinachorushwa na Redio
Magic FM ya jijini, Dar es
Salaam ambapo alitakiwa
kuelezea kipindi cha uongozi
wa rais huyo ambaye
amebakiza miaka miwili
madarakani.
Akijibu swali hilo, Zitto
alisema kiongozi huyo wa nchi
anapaswa kuheshimiwa
kutokana na uamuzi wake wa
kuruhusu uhuru wa maoni
tofauti na ilivyo kwa viongozi
wengi duniani.
Mbunge huyo alisema,
huchukia watu wanaposema,
Rais Kikwete ni dhaifu na
kuwataka kutotumia vibaya
uhuru wa kutoa maoni.
“Naomba nisieleweke vibaya,
lakini ukweli ni kwamba, Rais
Kikwete ameacha kiasi
kikubwa uhuru wa watu kutoa
maoni. Sasa rais anaweza
kutukanwa lakini yeye
hachukii. Ni vema wananchi
wakaacha kutumia vibaya
uhuru huo.
“Kikwete ni mkuu wa nchi
aliyejaribu kwa kiasi kikubwa
kuwafanya watu kuwa huru.
Kama rais angekuwa ni mtu
mwenye hasira, ni wazi
kwamba nchi ingekuwa katika
machafuko makubwa,”
alibainisha Zitto.
Pia alimwagia sifa, Rais
Kikwete kwa kuimarisha
uhusiano wa kimataifa na
kuwezesha katika kipindi
kifupi viongozi wawili wa
mataifa makubwa kuja nchini.
“Rais ame balance (ameweka
uwiano sawa) wa uhusiano wa
kimataifa. Tunashuhudia
ndani ya miezi mitatu marais
wawili wanakuja nchini yani
Rais wa China, Xi Jinping
ambaye alikuja mapema
mwaka huu na Rais wa
Marekani, Barack Obama
anayetarajia kuja nchini, Julai
Mosi mwaka huu,” alisema
mbunge huyo.
Mbali na sifa hizo,
alimtahadharisha rais kuwa
anapaswa kuwa makini na
watu aliowaita wafaidhina
ambao wanateka watu
maarufu wakiwamo waandishi
wa habari.
Alisema watu hao wanaweza
kufuta sifa za uongozi wa Rais
Kikwete kutokana na tabia
iliyoanza kujengeka nchini
hususan ya utekaji, kung’oa
kucha na kutoa macho kama
alivyofanyiwa Mhariri
Mtendaji wa New Habari,
Absolom Kibanda.
“Matukio yanayoendelea
nchini yanaweza
kumwondolea sifa rais. Sasa
tunashuhudia waandishi
wanaanza kuuawa na wengine
kuzuriwa ni vema akakemea
vitendo hivyo visiendelee
kuwepo ndani ya jamii yetu,”
alisema.
Zitto alimtaka rais
kuhakikisha vurugu za kidini
ambazo zimeanza kuchipukia
nchini zinakomeshwa kwa
nguvu zote ili Watanzania
waendelee kuishi kwa
kupendana kama ilivyokuwa
miaka iliyopita.
“Kuhusu suala la udini na
vitendo vya rushwa,
namuomba Rais Kikwete awe
mkali kwa kuvidhibiti. Iwapo
vitadhibitiwa mapema ni wazi
atamaliza uongozi wake na
heshima kubwa,” alisisitiza
Zitto.
Habari: JAMBO LEO.
Post a Comment