ALIYEMUUA PADRE MUSHI SASA KUSAKWA KWA MIL.1O
https://menacotz.blogspot.com/2013/02/aliyemuua-padre-mushi-sasa-kusakwa-kwa.html
>> KWA YEYOTE ATAKAYETAJA BASI KUIBUKA NA HICHO KITITA
WAKATI
kukiwa na taarifa kwamba maofisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani
(FBI) wametua nchini kwa ajili ya kufanya upelelezi wa mauaji ya Padri
Evarist Mushi, Jeshi la Polisi limetangaza dau la Sh10 milioni kwa
atakayefichua aliyemuua padri huyo.Padri Mushi aliuawa kwa
kupigwa risasi Jumapili iliyopita wakati akienda kuongoza ibada katika
Kanisa la Mtakatifu Teresia lililopo Beit el Ras nje kidogo ya mji wa
Zanzibar, ambapo inadaiwa kuwa waliomuua walikuwa wamepanda pikipiki
aina ya Vespa na walimfyatulia padri huyo risasi tatu akiwa ndani la
gari yake.
Wakati
polisi wakitangaza dau hilo, Sheikh Ali Khamis Ali (65) mkazi wa Kitope
Kaskazini Unguja, aliuawa jana kwa kukatwa mapanga mjini Zanzibar,
baada ya wezi kuvamia shambani kwake.
Habari
za kuaminika zilizopatikana juzi zinaeleza kuwa maofisa hao wa FBI,
wako nchini na tayari na wamekutana na baadhi ya viongozi wa Serikali
kwa ajili ya kuanza kazi hiyo.
Chanzo
chetu cha habari kimeeleza kuwa maofisa hao walikutana na Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kwa ajili ya kuangalia ni
namna gani watafanya shughuli zao katika upelelezi huo.
Pamoja
na ushiriki FBI, taarifa zinaeleza kuwa maofisa wa Serikali ya Tanzania
wamezungumza na taasisi za upelelezi za nchi tano, ili kuongeza nguvu
katika upelelezi huo.
Taasisi
nyingine inayotajwa kuwa huenda ikashiriki katika uchunguzi huo ni
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Uingereza (Scotland Yard).
Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima alilithibitishia gazeti
hili kwamba Serikali imeanza kufanya mazungumzo na mashirika mbalimbali
ya upelelezi duniani kwa ajili ya kushirikiana nayo kuchunguza mauaji ya
Padri Mushi, lakini akasema kuwa ni mapema mno kuyataja.
“Tumefuata
maagizo aliyotoa Rais Kikwete kwamba tushirikishe mataifa mbalimbali
kuchunguza mauaji yaliyotokea Zanzibar, siwezi kutaja kwa majina, ila
tayari tumeanza kuzungumza na nchi mbalimbali,” alisema Silima.
Akizungumza
mjini Zanzibar jana, Kamishna wa Polisi visiwani humo, Mussa Ali Mussa
alisema kuwa hadi sasa hakuna mtu aliyefikishwa mahakamani kuhusiana na
tukio hilo la mauaji.
“Hakuna
aliyefikishwa mahakamani, lakini wapo watu ambao wamekamatwa
wakihusishwa na tukio hili na tunaendelea kuwahoji, wengine
tunawaachia,” alisema na kuongeza:
“Tumeahidi kutoa Sh10 milioni kwa mtu yeyote, atakayetoa taarifa za mauaji ya Padri Mushi, hii itakuwa kama zawadi tu.”
Post a Comment