MAFUTA YAZIDI KUPOROMOKA BEI
https://menacotz.blogspot.com/2015/01/mafutav-yazidi-kuporomoka-bei.html
Mabadiliko hayo ya bei, yanatokana na kushuka kwa bei za nishati hizo katika soko la dunia tangu Julai, mwaka jana.
Hata hivyo, kushuka kwa bei hizo hakuendani na hali halisi ya kiwango cha kushuka kwa gharama za nishati hizo nchini kulinganisha na bei za kipindi kilichopita na mabadiliko katika soko la dunia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Slaam kuhusu bei kikomo za mafuta aina ya petroli na mwenendo wa bei za mafuta nchini na katika soko la dunia, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, alisema bei za rejareja zitaanza kutumika katika vituo vinavyouza nishati hizo leo.
Alisema petroli imeshuka kwa Sh. 74 sawa na asilimia 3.63, dizeli Sh. 62 (asilimia 3.25) na mafuta ya taa Sh. 54 (asilimia 2.88) kwa lita.
Ngamlagosi alisema katika mabadiliko hayo, katika jiji la Dar es Salaam, petroli itauzwa kwa Sh. 1, 955, dizeli Sh. 1, 855 na mafuta ya taa Sh. 1, 833 kwa lita.
Katika jiji la Arusha, petroli itauzwa kwa Sh. 1,955, dizeli Sh. 1, 846, mafuta ya taa Sh. 1,833; Dodoma, petroli (Sh. 2,014), dizeli (Sh. 1,905), mafuta ya taa (Sh. 1,892); Iringa, petroli (Sh. 2,019), dizeli (Sh. 1,910), mafuta ya taa (Sh. 1, 897); Geita, petroli (Sh. 2,120), dizeli (Sh. 2,011), mafuta ya taa (Sh. 1,998) na Kigoma, petroli (Sh. 2,186), dizeli (Sh. 2,077) na mafuta ya taa ni (Sh. 2,064).
Alivitaka vituo hivyo kuchapisha bei za bidhaa hizo na punguzo kwenye mabango yanayoonekana bayana.
Alisema bei za mafuta masafi ya petroli katika soko la dunia imeshuka kwa takriban dola za Marekani 249 (asilimia 25) kwa tani, wakati dizeli dola 189 (28) na mafuta ya taa dola 180 (asilimia 24) kati ya Julai na Novemba, mwaka jana.
Ngamlagosi alisema kati ya Septemba, mwaka jana hadi Januari 15 mwaka huu, bei ya petroli katika soko la ndani imeshuka kwa jumla ya Sh. 311 kwa lita (asilimia 16); dizeli Sh. 244 (asilimia 13), huku mafuta ya taa yakishuka kwa Sh. 207 kwa lita, ambayo ni sawa na punguzo la asilimia 11.
Alisema katika kipindi hicho, thamani ya Shilingi ya Tanzania kulinganisha na ya dola ya Marekani, imeshuka kwa asilimia nne.
Ngamlagosi alisema bei ya nishati hizo zingepungua zaidi iwapo thamani ya Shilingi isingeendelea kushuka.
Hata hivyo, alisema kwa wastani bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji, huchangia asilimia 60 ya bei ya mafuta katika soko la ndani.
Hivyo, akasema asilimia ya kushuka katika soko la ndani haiwezi kuwa sambamba na ile ya ushukaji katika soko la dunia.
Ngamlagosi alisema kampuni zipo huru kuuza bidhaa hizo za mafuta kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya ile ya kikomo.
Alisema kati ya Septemba hadi Desemba, mwaka jana, bei za mafuta ghafi, zimekuwa zikishuka kwa kasi kwa wastani wa asilimia 40 kutoka Dola za Marekani 100 kwa pipa hadi wastani wa Dola 60 kwa pipa ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
Baadhi ya sababu za kushuka kwa bei hizo kwenye soko hilo zilielezwa kuwa ni kutokana na kudorora kwa uchumi wa Bara la Ulaya na hali ya kisiasa ‘geopolitics’ katika nchi za Marekani na Urusi
Post a Comment