MWANASPOTI::::KOPUNOVIC AIBADILISHA SIMBA SASA INA KASI, NGUVU
https://menacotz.blogspot.com/2015/01/mwanaspotikopunovic-aibadilisha-simba.html
Katika siku yake ya kwanza kwenye mazoezi ya timu
hiyo jana Ijumaa Kwenye Uwanja wa Ngome uliopo Fuoni, Kopunovic raia wa
Serbia aliyechukua nafasi ya Patrick Phiri wa Zambia, alitumia muda wa
dakika 90 kuanzia saa 10:00 hadi saa 11:30 jioni katika mazoezi, kisha
akafanya mkutano mdogo na wachezaji wake.
Kocha huyo aliwaelekeza wachezaji wake kufanya
mazoezi ya kukimbia kwa dakika 30 ili kutengeneza pumzi na stamina na
kisha akawasimamisha na kuwapa zoezi la kumiliki mpira huku wakikokota
jambo lililoonekana kupokelewa vizuri na wachezaji wake.
Baada ya mazoezi hayo Kopunovic alisema; “Najua
wachezaji wana mawazo ya kupoteza mechi ya kwanza, nimewataka wasahau
matokeo ya mechi hiyo kwani sasa tunajenga timu. Nataka wacheze soka la
kasi na pasi za haraka lakini viungo wakabe wasiruhusu wapinzani kupenya
katika eneo lao.
“Nataka kuirudishia timu uwezo wa kupambana kwa
dakika 90 kwani kwenye mechi yao na Mtibwa walicheza kwa dakika 30 tu
kisha wakapotea, ndiyo maana nimewafanyisha mazoezi ya kuongeza pumzi,”
alisema Kopunovic
Kocha huyo alisisitiza kwamba ili Simba iweze
kupata matokeo mazuri uwanjani ni lazima icheze soka la kasi, nguvu na
wachezaji wake wapambane kwa dakika 90 vinginevyo itaendelea kupata
matokeo yasiyoridhisha.
Simba imepoteza mechi mbili ndani ya wiki moja
kwani Desemba 26, mwaka jana ilifungwa bao 1-0 na Kagera Sugar katika
Ligi Kuu Bara halafu ikapoteza mchezo juzi Alhamisi dhidi ya Mtibwa kwa
bao 1-0 ikiwa ni mechi yao ya kwanza ya Kombe la Mapinduzi.
Wakati huohuo, Kopunovic ametangaza hali ya hatari
kwa wachezaji wa kigeni wa Simba ambao hawapo kikosini kwa ruhusa au
matatizo ambayo hayafahamiki na uongozi wakiwemo Juuko Murshid, Simon
Sserunkuma, Joseph Owino, Emmanuel Okwi na Joseph Owino wote raia wa
Uganda.
“Lazima timu iwe na nidhamu haiwezekani wachezaji
wote wanne wa kigeni wasiwepo na timu hapa, wao wanatakiwa kuwa tofauti
na wenzao wazawa. Nimeuambia uongozi nawahitaji na lazima waje,” alisema
Kopunovic.
Post a Comment