MWANANCHI; CCM, CUF WALIANZISHA DAR

Dar es Salaam. 
Utata mpya umeibuka kuhusu matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baada ya wagombea watatu waliotangazwa washindi kuwekwa kando ikidaiwa kuwa badala yake walioshindwa waliapishwa kuchukua nafasi zao, hali iliyozua vurugu kubwa zilizotulizwa na polisi kwa mabomu ya machozi Ubungo jana.
Kutokana na hali hiyo, wafuasi wa CUF wanaodai wagombea wa chama chao ndiyo walioshinda, waliibuka na kutanda nje ya Hoteli ya Landmark kupinga kuapishwa kwa baadhi ya wenyeviti wa Serikali za Mitaa wa CCM katika Wilaya ya Kinondoni, hatua iliyosababisha baadhi ya wagombea na mashabiki kushushiwa kipigo hadi polisi walipoingilia kati kwa kurusha mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya.
Vurugu hizo zilizodumu kuanzia saa tatu hadi saa tano asubuhi, zililenga kuzuia wateule watatu wa mitaa ya Ukwamani, Pakacha na King’ong’o kuapishwa kwa madai kuwa siyo walioshinda.
Kwa upande mwingine, aliyekuwa mgombea wa Mtaa wa Msisiri, Juma Mbena alivamia eneo hilo akidai kuwa Gasper Chambembe (CUF), ambaye alishinda katika mtaa huo hakustahili kuapishwa, kitendo kilichosababisha ashushiwe kipigo na wafuasi wa CUF.
Licha ya Mbena kupigwa na kuchaniwa nguo, pia Sultan Jetta (CCM) ambaye alitangazwa kushinda katika Mtaa wa Ukwamani, Kawe alizuiwa na wafuasi wa CUF kuapishwa, wakidai kuwa mgombea wao, Nasri Mohammed Mashaka ndiye aliyestahili kuapishwa. Alipogoma, walimkamata na kumshushia kipigo hadi alipookolewa na polisi.
Baadaye Jetta alirudishwa ukumbini chini ya ulinzi wa polisi na kuapishwa pamoja na wenyeviti wenzake 153 kati ya 191 wa Wilaya ya Kinondoni.
Aliyekuwa mgombea wa Mtaa wa Pakacha Kata ya Tandale, Hussein Juma Mpeka (CUF) alidai kuwa licha ya uchaguzi huo kuvurugika, alipewa barua ya kuitwa kuapishwa lakini baada ya kufika eneo hilo alikataliwa kuingia ukumbini, badala yake aliyeruhusiwa ni Nassib Omary Kalenga wa CCM.
Hali ilivyokuwa
Shughuli ya kuapisha wenyeviti hao ilianza saa mbili asubuhi na baada ya saa moja, wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo walikusanyika eneo hilo ili kushuhudia uapishwaji huo.
Kati yao walikuwapo viongozi wa vyama vya CCM na CUF wa Wilaya ya Kinondoni pamoja na wagombea walioeleza kuwa walishinda katika uchaguzi na matokeo yao kutangazwa lakini hawakupewa barua za uthibitisho kutoka kwa mamlaka husika.
Waendesha bodaboda na wananchi wanaofanya biashara zao kando ya hoteli hiyo nao walikusanyika kwa lengo la kushuhudia kinachoendelea hali iliyowafanya polisi waliokuwa katika magari mawili aina ya Landrover Defender kuwataka wananchi hao kuwa watulivu.
Mmoja wa wakazi wa Kawe, Anna Cheupe aliyekuwa eneo hilo alisema licha ya kuwa ni mwanachama wa CCM, hakufurahishwa na kitendo cha matokeo ya Mtaa wa Ukwamani kubadilishwa, kauli ambayo iliungwa mkono na watu waliokuwa karibu yake.

Related

SIASA 7281326328051258399

Post a Comment

ads by blogger

Follow Us

Hot in week

BLOG ZINGINE

BLOG OWNER

BLOG OWNER
MESHACK JACKSON

Side Ads

Instagram

JOIN US ON TWITTER

Text Widget

Millard Ayo – Official Website

item