WAKATI wadau wa tasnia ya habari wakihoji ubabe uliotumiwa na serikali kulifungia gazeti la wiki la MwanaHalisi kwa madai ya uchochezi, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assa Mwambene, amembebesha sakata hilo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto.

Mwambene katika kuivua lawama serikali, alidai kuwa Zitto alikuwa mtu wa kwanza baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, aliyemtahadharisha asiende ofisini kumchekea Mkurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi, wachapishaji wa MwanaHalisi, Said Kubenea ili isije kumharibia kazi.

Serikali ililifungia gazeti la MwanaHalisi Julai 30 mwaka jana, kutochapisha nakala yoyote kwa muda usiojulikana kwa madai ya kuandika habari na makala ya uchochezi.MwanaHalisi ndilo gazeti lililoandika kwa undani tukio zima la watu wanaoshukiwa kumteka kumpiga, kumng’oa meno na kisha kumtelekeza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madakatari nchini, Dk. Stephen Ulimboka.

Mwambene ambaye aliteuliwa kushika nafasi hiyo kutoka kwa Clement Mshana aliyehamishiwa TBC, alijikuta akitoa siri hiyo Ijumaa iliyopita wakati wa kongamano la kutimiza miaka 50 ya Redio ya Ujerumani ‘Deutsche Welle’ (DW) Idhaa ya Kiswahili lililofanyika kwenye Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ilikuja baada ya kubanwa kwa maswali yaliyokuwa yanamshutumu yeye na serikali yake kubana uhuru wa vyombo vya habari, huku baadhi ya washiriki wakiinyooshea kidole cha moja kwa moja serikali katika suala zima la kulifungia MwanaHalisi ili lisizidi kuwaumbua.

Katika utetezi wake, Mwambene alisema serikali haizuii uhuru huo, na hata hatua ya kufungiwa kwa baadhi ya magazeti ni kwa sababu ya kulinda hadhi ya nchi.
Alitolea mifano nchi za Magharibi zinazodaiwa kuwa na demokrasia kuwa nazo zinafungia au kuvifuta vyombo vya habari vyenye mwelekeo wa uchonganishi.
Alisema kwa mara ya kwanza akiwa mkurugenzi wa idara hiyo, alipofika bungeni kujitambulisha kwa wabunge, aliitwa pembeni na Zitto, na kutahadharishwa juu ya MwanaHalisi.

“Mnasema sisi tunaminya uhuru wa vyombo vya habari kwa kutolea mifano nchi za Uingereza na Marekani…mnaweza kuniambia leo Assange, yule mmiliki wa mtandao wa Wikileaks yuko wapi au gazeti la News of the World lilipo? Haya mambo yanafanyika hata katika nchi mnazozisifia kuwa na demokrasia.

“Na niseme kabisa nilipokwenda bungeni kama Mkurugenzi wa Idara ya Habari - Maelezo, Zitto aliniita pembeni na kuniambia katika kazi yangu mpya nisiende kumchekea Said Kubenea,” alisema Mwambene.

Kauli hiyo ilizua minong’ono kutoka kila kona ya ukumbi huo, huku baadhi ya washiriki wakisema serikali inatafuta sehemu ya kufichia udhaifu na ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari kwa kuwahusisha baadhi ya watu na uamuzi wa kuminya uhuru huo.

Tanzania Daima lilimtafuta Zitto kujua msimamo wake kuhusu kauli hiyo ya Mwambene katika suala zima la kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi, lakini akajibu kwa kifupi kuwa hausiki.

“Sasa mimi ni mwajiri wake? Hayo maneno ni ya kutuchonganisha tu hayo, mimi nina nguvu gani ya kusema hivyo? Inaingia akilini kweli?” alijibu Zitto kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu yake ya mkononi.

Hata hivyo, Mwambene aliwashangaza waliohudhuria kongamano hilo baada ya kusema kuwa serikali imetoa uhuru mkubwa wa habari ambapo baadhi huitukana serikali, lakini hawafanywi kitu.

Baadhi ya wageni wengine walioalikwa kama wazungumzaji wakuu na kutia fora, ni nguli wa habari nchini, Jenerali Ulimwengu, mwanablog mahiri Majjid Mjengwa, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Valerie Msoka na Naibu Mkuu wa Idhaa DW, Mohamed Abdulrahman.

Sakata la kufungiwa kwa gazeti hilo kwa sasa limezidi kuwa tata kutokana na Rais Jakaya Kikwete kunukuliwa hivi karibuni akiwa mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kuwa hatalifungulia kamwe kutokana na kosa la kuchochea. Pamoja na kwamba hakulitaja kwa jina, lakini kwa sasa nchini gazeti hilo ndilo limefungiwa kwa kosa hilo la kudaiwa kuchochea.

Kutokana na msimamo huo wa Rais Kikwete, Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT) hivi karibuni kilikutana na kujadili sakata hilo na kuteua kamati ya wajumbe wa kukutana na rais kumshauri.

Wajumbe hao wataongozwa na Mwenyekiti wa MOAT, Reginald Mengi ili kukutana na Rais Kikwete ambaye wanaamini kwa sasa ndiye pekee anaweza kutoa uamuzi wa kufunguliwa kwa gazeti hilo.