Tanzania Daima: Zitto ahusishwa kifungo cha MwanaHalisi
https://menacotz.blogspot.com/2013/02/tanzania-daima-zitto-ahusishwa-kifungo.html
WAKATI wadau wa tasnia ya habari wakihoji ubabe uliotumiwa na serikali
kulifungia gazeti la wiki la MwanaHalisi kwa madai ya uchochezi,
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assa Mwambene, amembebesha
sakata hilo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto.
Mwambene katika kuivua lawama serikali, alidai kuwa Zitto alikuwa
mtu wa kwanza baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo,
aliyemtahadharisha asiende ofisini kumchekea Mkurugenzi wa Kampuni ya
Hali Halisi, wachapishaji wa MwanaHalisi, Said Kubenea ili isije
kumharibia kazi.
Serikali ililifungia gazeti la MwanaHalisi Julai 30 mwaka jana,
kutochapisha nakala yoyote kwa muda usiojulikana kwa madai ya kuandika
habari na makala ya uchochezi.MwanaHalisi ndilo gazeti lililoandika
kwa undani tukio zima la watu wanaoshukiwa kumteka kumpiga, kumng’oa
meno na kisha kumtelekeza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madakatari nchini,
Dk. Stephen Ulimboka.
Mwambene ambaye aliteuliwa kushika nafasi hiyo kutoka kwa Clement
Mshana aliyehamishiwa TBC, alijikuta akitoa siri hiyo Ijumaa iliyopita
wakati wa kongamano la kutimiza miaka 50 ya Redio ya Ujerumani
‘Deutsche Welle’ (DW) Idhaa ya Kiswahili lililofanyika kwenye Ukumbi wa
Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo ilikuja baada ya kubanwa kwa maswali yaliyokuwa
yanamshutumu yeye na serikali yake kubana uhuru wa vyombo vya habari,
huku baadhi ya washiriki wakiinyooshea kidole cha moja kwa moja
serikali katika suala zima la kulifungia MwanaHalisi ili lisizidi
kuwaumbua.
Katika utetezi wake, Mwambene alisema serikali haizuii uhuru huo,
na hata hatua ya kufungiwa kwa baadhi ya magazeti ni kwa sababu ya
kulinda hadhi ya nchi.
Alitolea mifano nchi za Magharibi zinazodaiwa kuwa na demokrasia
kuwa nazo zinafungia au kuvifuta vyombo vya habari vyenye mwelekeo wa
uchonganishi.
Alisema kwa mara ya kwanza akiwa mkurugenzi wa idara hiyo,
alipofika bungeni kujitambulisha kwa wabunge, aliitwa pembeni na
Zitto, na kutahadharishwa juu ya MwanaHalisi.
“Mnasema sisi tunaminya uhuru wa vyombo vya habari kwa kutolea
mifano nchi za Uingereza na Marekani…mnaweza kuniambia leo Assange,
yule mmiliki wa mtandao wa Wikileaks yuko wapi au gazeti la News of
the World lilipo? Haya mambo yanafanyika hata katika nchi mnazozisifia
kuwa na demokrasia.
“Na niseme kabisa nilipokwenda bungeni kama Mkurugenzi wa Idara ya
Habari - Maelezo, Zitto aliniita pembeni na kuniambia katika kazi
yangu mpya nisiende kumchekea Said Kubenea,” alisema Mwambene.
Kauli hiyo ilizua minong’ono kutoka kila kona ya ukumbi huo, huku
baadhi ya washiriki wakisema serikali inatafuta sehemu ya kufichia
udhaifu na ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari kwa kuwahusisha
baadhi ya watu na uamuzi wa kuminya uhuru huo.
Tanzania Daima lilimtafuta Zitto kujua msimamo wake kuhusu kauli
hiyo ya Mwambene katika suala zima la kufungiwa kwa gazeti la
MwanaHalisi, lakini akajibu kwa kifupi kuwa hausiki.
“Sasa mimi ni mwajiri wake? Hayo maneno ni ya kutuchonganisha tu
hayo, mimi nina nguvu gani ya kusema hivyo? Inaingia akilini kweli?”
alijibu Zitto kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu yake ya mkononi.
Hata hivyo, Mwambene aliwashangaza waliohudhuria kongamano hilo
baada ya kusema kuwa serikali imetoa uhuru mkubwa wa habari ambapo
baadhi huitukana serikali, lakini hawafanywi kitu.
Baadhi ya wageni wengine walioalikwa kama wazungumzaji wakuu na
kutia fora, ni nguli wa habari nchini, Jenerali Ulimwengu, mwanablog
mahiri Majjid Mjengwa, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania (Tamwa), Valerie Msoka na Naibu Mkuu wa Idhaa DW,
Mohamed Abdulrahman.
Sakata la kufungiwa kwa gazeti hilo kwa sasa limezidi kuwa tata
kutokana na Rais Jakaya Kikwete kunukuliwa hivi karibuni akiwa mjini
Addis Ababa nchini Ethiopia kuwa hatalifungulia kamwe kutokana na kosa
la kuchochea. Pamoja na kwamba hakulitaja kwa jina, lakini kwa sasa
nchini gazeti hilo ndilo limefungiwa kwa kosa hilo la kudaiwa
kuchochea.
Kutokana na msimamo huo wa Rais Kikwete, Chama cha Wamiliki wa
Vyombo vya Habari nchini (MOAT) hivi karibuni kilikutana na kujadili
sakata hilo na kuteua kamati ya wajumbe wa kukutana na rais kumshauri.
Wajumbe hao wataongozwa na Mwenyekiti wa MOAT, Reginald Mengi ili
kukutana na Rais Kikwete ambaye wanaamini kwa sasa ndiye pekee anaweza
kutoa uamuzi wa kufunguliwa kwa gazeti hilo.
Post a Comment